Home KITAIFA SERIKALI KUPITIA TPA KUTUMIA ZAIDI YA BILIONI 100 KUBORESHA BANDARI ZA ZIWA...

SERIKALI KUPITIA TPA KUTUMIA ZAIDI YA BILIONI 100 KUBORESHA BANDARI ZA ZIWA TANGANYIKA

Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula akiwaelezea utendaji kazi wa bandari za ukanda wa ziwa Victoria
Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula akiwaelezea utendaji kazi wa bandari za ukanda wa ziwa Victoria

 

Na Mwandishi wetu, Kigoma

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iwekeza zaidi ya shilingi bilioni 800 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kuboresha bandari katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuongeza maradufu kiwango cha utendaji kazi, uwezo wa kuhudumia mizigo pamoja na abiria.

Kwa upande wa ziwa Tanganyika, TPA imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuboresha bandari za ukanda wa ziwa hilo ambazo ni mahususi kwa shughuli za usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kwenda nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Juni 02, 2023 na Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula akiongea na waandishi wa habari na kubainisha kuwa shehena zinazohudumiwa kwa wingi katika bandari hizo ni vyakula na vifaa vya ujenzi hususani saruji.

Mabula ameongeza kuwa, Bandari ya Kigoma ndio bandari kongwe na kubwa kuliko bandari zote za ukanda wa Ziwa Tanganyika ambapo hadi kufikia mwezi Mei, mwaka huu imeweza kuhudumia tani 131,000 ya shehena ya mzigo mbalimbali sawa na asilimia 48 ya shehena zote zinayohudumiwa katika bandari zote za ukanda wa ziwa hilo zipatazo tani 273,000.

Mwonekano wa picha tofauti za vifaa vya kisasa vya kupakua na kupakia mizigo katika bandari ya Kigoma kama vilivyokutwa na mpiga picha wetu leo Juni 02, 2023

 

Vilevile Mabula amesema, kiasi cha shilingi bilioni 32.5 kitatumika kwa ajili uboreshaji wa bandari za Kibirizi na Ujiji zilizopo katika Mkoa wa Kigoma kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa majengo ya abiria, jengo la bandari, ujenzi wa ofisi za wadau, sehemu za kuhifadhia mizigo pamoja na gati lenye urefu wa mita 256 kwa ajili ya kapakia na kupakua mzigo katika bandari ya Kibirizi.

Mwonekano wa ujenzi wa gati jipya katika bandari ya Kibirizi iliyopo katika manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma ukiwa unaendelea

Akielezea mchango wa bandari ya Kigoma katika kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, Meneja Mabula amesema

“Asilimia 80 ya mizigo inayohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam inakwenda nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na katika mizigo hiyo, asilimia 48 husafirishwa kupitia bandari ya Kigoma na hivyo kuchangia kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam”

Kufuatia hilo, Mabula ametoa wito kwa wananchi, wadau wa bandari na sekta binafsi kuchangamkia fursa zinazotokana na uboreshaji wa bandari za za ziwa Tanganyika unaofanywa na TPA ikiwemo fursa za kuwekeza katika vyombo vya usafiri.

Naye Mhandisi wa mradi wa uboreshaji wa bandari za Kibirizi na Ujiji, Mhandisi Elly Mtaki amesema, baada ya kukamilika kwa mradi huo ufanisi utaongezeka katika upakuaji na upakiaji wa mizigo na hiyo ni kufuatia ujenzi wa gati jipya linalojengwa katika bandari ya Kibirizi.

Mhandisi wa Mradi wa uboreshaji wa bandari za Kibirizi na Ujiji, Mhandisi Elly Mtaki akiwaelezea waandishi habari maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo leo Juni 02, 2023

Wakiongea kwa nyakati tofauti, mawakala wa forodha katika bandari ya Kigoma Mbaraka Said na Brian William wameonesha kuridhishwa na utendaji kazi wa bandari hususan ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwa watendaji na wafanyakazi wa bandari, muda unaotumika kuhudumia shehena na uwepo wa mashine za kupakua na kupakia mizigo katika bandari hiyo.

Mbaraka Said ambaye ni Wakala wa Forodha katika bandari ya Kigoma akiongea na waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wao katika bandari ya Kigoma
ambaye ni Wakala wa Forodha katika bandari ya Kigoma, Brian William akiongea na waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wao katika bandari hiyo leo Juni 02, 2023

Ziwa Tanganyika lipo katika mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi na Rukwa. Bandari kuu zilizopo katika ziwa hili ni bandari ya Kigoma, Kibirizi, Kipili, Kasanga, Kagunga, Kabwe na Kirando.
Bandari ya Kigoma ambayo ni bandari kongwe katika ukanda wa ziwa hilo imeunganishwa kwa barabara na reli, ambapo ina vifaa vingi vikiwemo mizani, matanki ya mafuta, karakana na eneo la kupumzikia abiria.

Previous articleSAMIA AIBUA HOFU CHADEMA, ACT… MAPINDUZI YA MAENDELEO YAWAPA MTIHANI _ MAGAZETINI LEO IJUMAA JUNI 02/2023
Next articleWATALII WA UWINDAJI WA KITALII WAONGEZEKA NCHINI, REKODI YAVUNJWA HAIJAWAHI KUTOKEA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here