Home KITAIFA SERIKALI KUPITIA TANROADS YASAINI MIKATABA MIWILI YA MIRADI YA KIMAKAKATI MKOANI SINGIDA

SERIKALI KUPITIA TANROADS YASAINI MIKATABA MIWILI YA MIRADI YA KIMAKAKATI MKOANI SINGIDA

Serikali kupitia TANROADS imesaini mikataba miwili ya ujenzi wa barabara unganishi katika Daraja la Sibiti yenye urefu wa kilometa 24.83 kwa kiwango cha lami (mradi unatekelezwa Wilaya ya Mkalama) na mkataba wa ujenzi wa barabara ya Makongolosi – Rungwa – Itigi – Mkiwa sehemu ya Noranga – Doroto yenye urefu wa kilometa 6 na Itigi – Mkiwa yenye urefu wa kilometa 25.569 kwa kiwango cha lami, Mradi ambao utatekelezwa katika Wilaya ya Itigi.

Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji Saini wa mikataba hiyo miwili leo Mei 14- 2023 Wilayani Itigi mkoani Siginda, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof: Makame Mbarawa amesema lengo la miradi hiyo ambayo inajengwa kwa kutumia fedha za ndani kwa 100% ni kuwaondolea wananchi kero ya usafiri wa barabarani na kuboresha mtandao wa barabara na madaraja ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji hivyo kukuza uchumi wa Nchi.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi

Amesema Serikali imelenga kuendelea na kukamilisha mkakati wake wa kuunganisha mikoa kwa barabara za lami ambapo kwa miradi ambayo mikataba imesainiwa leo “tunaelekea kuiunganisha Singida na Mbeya na kwa upande mwingine mikoa ya Singida na Simiyu na kwamba Ujenzi wa barabara unganishi katika Daraja la Sibiti utakapokamilika pia utasaidia kuondoa adha ya usafirishaji wa mizigo na abiria na kuongeza usalama kwa wote watakaotumia daraja hilo pamoja na kukuza biashara mbalimbali”

“Barabara unganishi katika daraja hili zitasaidia pia kuunganisha na kuboresha hali ya usafiri wa wananchi wetu na usafirishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo, mifugo na mazao ya misitu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Singida pamoja na mikoa jirani ya Manyara, Simiyu, Shinyanga, Arusha, Dodoma na Tabora kwenda maeneo mbalimbali ya nchi yetu” ameongeza Waziri Pro: Mbarawa.

Ameongeza kuwa vile vile Serikali imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara kutoka Mbeya hadi Makongolosi (km 111), hivyo ujenzi wa barabara ya Itigi hadi Mkiwa ambayo ni sehemu ya barabara inayotoka Mbeya kupitia Makongolosi – Rungwa – Itigi hadi Mkiwa utapunguza muda na gharama za safari kwa wananchi na bidhaa mbalimbali kutoka mikoa ya kanda ya ziwa kwenda katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Katavi na Rukwa pamoja na nchi jirani za Zambia, Kongo na Malawi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo Mtendaji Mkuu TANROADS Eng: Rogatus Mativila amesema barabara hizo za maingilio ni kiungo muhimu kati ya wilaya ya Mkalama na wilaya zingine katika mkoa wa Singida, zinaungana na mtandao wa barabara muhimu za mkoa wa Singida ambazo zinaunganisha moja kwa moja mkoa huo na mikoa ya Simiyu, Manyara na hivyo kuunganisha na mikoa mingine jirani na Singida ya Shinyanga, Arusha, Tabora na Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila akongea wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba ya ujenzi wa miundombinu ya barabara mkoani Singidau

Amesema kuwa TANROADS ilisaini mkataba na kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Makongolosi – Rungwa – Itigi – Mkiwa, Sehemu ya kutoka Noranga hadi Itigi (Mlongoji) yenye urefu wa Km 25 kwa kiwango cha lami kwa Gharama ya Shilingi bilioni 29.77, kwa sasa Mkandarasi yupo katika eneo la kazi na Ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri, Ujenzi umefikia 29%.

Eng: Mativila ameongeza kuwa Ujenzi wa barabara sehemu ya Noranga hadi Doroto (Km 6) na Itigi hadi Mkiwa (km 25.569) kwa kiwango cha lami unaohusisha jumla ya KM 31.569, unajengwa pia na Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 39.988 kwa kipindi cha miezi 19, ambapo barabara hizo za maingilio zitakapokamilika zitaondoa adha ya usafiri katika eneo korofi karibu na Daraja la Sibiti na hivyo kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi kama vile usafirishaji wa bidhaa pamoja na uwezeshaji wa shughuli za kijamii kwa ujumla.

Previous articleWAZIRI MKUU ALIA NA JAMII MMOMONYOKO WA MAADILI
Next articleMHE.TAUFIQ: MIMBA ZA UTOTONI BADO NI CHANGAMOTO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here