Home KITAIFA SERIKALI KUJENGA MASOKO MATANO YA MAZAO HALMASHAURI YA SONGEA

SERIKALI KUJENGA MASOKO MATANO YA MAZAO HALMASHAURI YA SONGEA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho awaomba wananchi kuchangamkia fursa za uchumi zitakazo chochewa na ujenzi wa Masoko ya Mazao yanayotarajiwa kujengwa na Halmashauri ya wilaya ya Songea.

Juhudi hizo za serikali zitakuza uchumi kwa wananchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa serikali.

Wito huo umetolewa katika ziara yake ya kutembelea na kujionea miradi ya maendeleo katika Jimbo la Peramiho Halmashauri ya wilaya ya Songea wakati akizungumza na wananchi katika matukio tofauti katika kata mbili za Mbingamwalule na Peramiho leo tarehe 18/07/2023.

“Tumepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa masoko ya mazao tutajenga soko kubwa Peramiho; Tutajenga Mpitimbi, tutajenga Matimila, tutajenga Mbingamwalule, na tutajenga katika kijiji cha Muhukuru,” alisisitiza Mhe, Mhagama

Alifafanua kwamba Ujenzi wa Miundo mbinu ya barabara ya Lami kuanzia kata ya Mbingamwalule inayoenda mpaka Kizuka ni ufunguzi wa Uchumi kutoka Mpaka wa Tanzania na Msumbiji na utasaidia kutoa mazao shambani kwenda kwenye masoko ya mazao.

Waziri Mhagama amesema, serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Songea imepanga kuunganisha kituo cha mabasi kitakachojengwa kata ya Mbingamwalule ili kusaidia wageni kupata urahisi wa kufika kwenye soko la mazao lilopo kwenye kata hiyo, na hivyo kufungua fursa mbalimbali za uchumi.

Akizungumzia kuhusu Mradi wa soko la kisasa uchuuzi wa mahitaji madogo madogo ya nyumbani lilojengwa kijiji cha Peremiho “A” ujenzi uliotekelezwa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) amesema nimefurahi kuona wafanyabiashara wanafanya shughuli zao katika eneo zuri na bora la kibiashara.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Mhe. Menas Komba amesema ujenzi wa soko la mazao katika kijiji cha Matomondo kata Mbingamwalule Halmashauri ilipokea jumla ya shilingi milioni 198 ambayo inatekeleza mradi na ujenzi unaendelea.

“Tunataka kukamilisha ujenzi wa vyoo ili tuwalete wachuuzi waliopo mtaani kwenye soko, waanze kuzoea kutumia soko jipya la mazao wakati tukimalizia ujenzi kwenye baadhi ya maeneo ya soko,” alisema Mhe.Menas

Alifafanua, ujenzi wa masoko hayo utasaidia kupunguza gharama za usafirshaji kutoka shambani mpaka kwenye eneo la soko.

“Tunafanya kazi kimkakati, hakuna mradi utakaoanzishwa usikamilike kila mradi utakaoletewa fedha lazima ukamilike kwa sababu sisi tunasimamia,” alisema Mhe. Menas

Katika hatua nyingine, Mhe, Menas ametoa ombi kwa serikali kufikiria kufanya Mji wa Peramiho kupata hadhi ya mji mdogo.

Naye Afisa Mtendaji wa kijiji cha Peramiho “A” Bi, Sara Athumani amesema soko la kujipatia mahitaji madogo madogo la Peramiho “A” limegharimu kiasi cha Milioni 185 ambazo zilikuwa zikisimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa ajili ya kuendeleza soko hilo, lenye ukubwa wa vizimba 82.

“Wananchi wametoka katika adha ya kupanga bidhaa kwenye vichanja na kuweka kwenye vizimba na kusaidia kuongeza mapato ya kijiji alisema,” Bi, Sara.

Kwa upande wake Bi, Modesta Melinga Mfanyabiashara wa soko la Peramiho “A” amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi wa soko zuri na kuwaweka sehemu sahihi ya kufanya biashara.

Previous articleSAMIA CUP YAANZISHWA MBEYA, BENS CO.LTD YAJITOSA KUDHAMINI
Next articleWELEDI WATAKIWA WAKATI WA KUFANYA UTAFITI WA UKATILI DHIDI YA WATOTO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here