Home KITAIFA SAMIA CUP YAANZISHWA MBEYA, BENS CO.LTD YAJITOSA KUDHAMINI

SAMIA CUP YAANZISHWA MBEYA, BENS CO.LTD YAJITOSA KUDHAMINI

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Katika kuibua na kukuza vipaji na Sekta ya michezo kwa ujumla, Serikali mkoani Mbeya imeanzisha ligi ya mpira wa miguu iliyopewa jina la Mbeya Samia Super Cup inayofanyika Wilayani Chunya.

Akizungumza na waandishi habari Ofisini kwake mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera amesema timu nane zinashiriki mashindano ya Mbeya Samia Super Cup kutoka Halmashauri zote za mkoa wa Mbeya.

Pia amesema kilele cha mashindano hayo kinatarajiwa kuwa Julai 25, 2023 lakini pia mkoa utaendesha ligi nyingine ya Mbeya Pre Season itakayofanyika wilayani Kyela lengo likiwa ni kupata wachezaji watakaosajiliwa kwenye timu za ligi kuu.

Homera amesema pia vilabu kutoka Zambia na nyingine tatu kutoka nchini Malawi na timu ya Dodoma jiji zimealikwa kushiriki mashindano hayo ambapo zitakutana na timu mbalimbali ikiwemo Ihefu.

Michezo hiyo imedhaminiwa na Kampuni ya Bens Agro star inayojihusisha na uuzaji na usambazaji Mbolea na madawa ya Kilimo ambapo Meneja wa kampuni hiyo Kanda ya Nyanda za juu kusini Israeli Mwampondele kwa niaba ya Mkurugenzi wake Benson Mwalunenge amesema wameamua kudhamini michezo hiyo ili kuiunga mkono Serikali katika juhudi mbalimbali ikiwemo kwenye sekta ya michezo nchini ambayo pia imeajiri vijana wengi.

Afisa michezo mkoa wa Mbeya Robert Mfugale amesema mpango wa Serikali ni kuona vijana wanajiajiri kwenye michezo ili kuendesha maisha yao na kuimarisha afya za vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa.

Michezo ni Sekta ambayo kwa sasa imeajiri vijana wengi hapa nchini licha ya kwamba changamoto kubwa hasa kwa vijijini ni uwepo wa vijana wazuri ambapo licha ya uzuri wao lakini wamekuwa wakishindwa kufika mbali kimichezo kutokana na sababu mbalimbali hasa kutoungwa mkono ili kufika hatua za juu hivyo serikali mkoani Mbeya inafanya juhudi hizi ili kuungana na baadhi ya wadau ambao wamekuwa wakijitokeza kukuza michezo katika maeneo yao.

Previous articleNAIBU WAZIRI NDERIANANGA AWATAKA WATANZANIA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA
Next articleSERIKALI KUJENGA MASOKO MATANO YA MAZAO HALMASHAURI YA SONGEA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here