Safari za Magari yaendayo haraka (Mwendokasi) kutoka Gerezani hadi Mbagala zinaanza rasmi leo kuelekea msimu wa Maonesho ya kimataifa ya Biashara ya 47 (Sabasaba) ambapo jumla ya magari 30 yataanza kutoa huduma.
Safari hizo zinazoanza leo gharama ya nauli ni Sh 750 kwa tiketi ambazo pia zitatolewa kwa njia ya mtandao kupitia application ya DART.
Akizungumza wakati wa kuzindua safari hiyo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Deusdelity Casmir amesema wataongeza watumiaji wa magari hayo kwa asilimia 50 ambapo pia wataanza na magari 20 kwa siku ya leo na kuendelea kuongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amewataka DART kuongeza muda wa safari za mabasi hayo kwa saa 24 ili wananchi waweze kupata huduma za usafiri kwa wakati wote.
“Mradi ulianza kutekelezwa kwa awamu ya kwanza inayoanzia Kimara hadi Kivukoni na matawi yake ya Morocco Magomeni na Fire Gerezani, Awamu ya pili ni hii ya kuja Mbagala , na Awamu ya tatu ni kuelekea Gongolamboto ambazo zote zimetumwa fedha nyingi na zinazotolewa na serikali na hapa ni sehemu muhimu kwani Mbagala inawatu wengi watu wamejua kuzaa na kuongezeka na vituo vimeongezeka pia,” ameeleza.
Katika Safari hiyo inayoanzia Kariakoo Gerezani hadi kituo kikuu cha Mabagala (terminal) vitatumika pia vituo vinne vya Kati ambavyo ni Sabasaba, Mission,Zakhem na Mbagala rangitatu .