NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Wakili wa kujitegemea Boniface Mwabukusi ameachiwa huru majira ya saa 12 jioni (Julai 14, 2023) baada ya kuhojiwa kwa zaidi ya saa saba katika Ofisi ya makao kikuu ya Polisi mkoa wa Mbeya.
Akizungumza na Jambo TV baada ya kumaliza mahojiano yake na polisi, Mwabukusi amesema aliitwa na Jeshi hilo akituhumiwa kwa makosa ya kutoa lugha ya chuki dhidi ya Waziri mkuu Kassim Majaliwa akidaiwa kwamba alihamasisha jamii kuwa Waziri Mkuu asiaminike kwa wananchi juu Suala la uwekezaji wa bandari kuwa una faida, hoja anazosema amezitolea maelezo polisi.
Aidha, Mwabukusi amesema kuitwa na kuhojiwa kwake kwa muda mrefu wa zaidi ya saa saba kunampa nguvu pamoja na mawakili wenzake kuendelea kuwatetea walalamikaji ambao wananchi waliofungua kesi ya kupinga mkataba wa Bandari kwa madai kuwa hauna maslahi kwa Taifa.
“Niwaambie tu kwamba kwa hili la kuitwa na kuhojiwa inanipa moyo sana na sikati tamaa pamoja na wenzangu, msimamo wangu uko palepale, inanipa moyo kwani naelewa kwamba kumbe Meseji Sent and Derivery (Ujumbe umeenda na umewafikia)”, Wakili Mwabukusi.
“Mimi ninachotaka kuwaambia wa-Tanzania ‘Hatujakosea’, tuko sahihi, msimamo wetu ni uleule na tupo tayari kufika kwenye vyombo vya kisheria kwa namna yoyote kwasababu ninaamini tutapita tena na tena kwenye uvuli wa mauti lakini tutafika kwenye ukombozi kamili”, Wakili Mwabukusi.
“Tuna haki za kikanuni na kikatiba, na mtu yeyote asiyetaka kukosolewa aondoke kwenye Ofisi za umma akakae nyumbani kwake hatutamfuata lakini mtu anayevunja Katiba tutamsema, kwahiyo siogopi, hata mtu akiwa Mbunge, Waziri mkuu au Rais hiyo ni dhamana hii nchi ninyetu sote sio ya watu wachache lazima nisimamie msimamo wangu lakini na kulinda raslimali za Taifa kwa mujibu wa Katiba”, Wakili Boniface Mwabukusi
Naye Wakili wa Mwabukusi kwenye shauri hilo Wakili Phillip Mwakilima amewashukuru wanasheria mbalimbali walioshirikiana katika sakata la kuhojiwa kwa mteja wake (Boniface Mwabukusi) akiwemo Rais wa TLS na Balozi Dkt. Wilbroad Slaa.
Amesema Mwabukusi ameamriwa kuripoti tena polisi mwanzoni mwa juma lijalo.
Hata hivyo Wakili Mwakilima amesema wamejiandaa kumfungulia mashtaka Juma Homera ambaye ni mkuu wa mkoa wa Mbeya kwa madai kuwa amewadhihaki wateja wao (Waliofungua kesi ya bandari) kuwa wanawatetea wezi pia anadaiwa kushindwa kusimamia nafasi yake ya Mwneyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama badala yake amesikika akisema waliofungua kesi ya kupinga mkataba wa Bandari anawakabidhi kwa machifu wa kimila ili wawashughulikie.
“Kwahiyo niiombe mamlaka yake (Mkuu wa mkoa Mbeya Juma Homera), Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ampeleke kwingine kama si kumuondoa kabisa maana kwa hili tu (kuwakabidhi waliofungua kesi kwa machifu) hafai kuwa mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama”, Wakili Phillip Mwakilima.
Mtuhumiwa Wakili Boniface Mwabukusi aliingia polisi saa 3:58 asubuhi na mahojiano yalimalizika majira ya saa kumi na dakika kadhaa lakini Wakili Mwakilima alieleza kuwa bado Mwabukusi anaendelea kuwa mikononi mwa Polisi licha ya kumaliza mahojiano hadi baadaye majira ya saa moja kasoro baada ya taratibu nyingine kukamilika hasa za kujidhamini hadi atakaporipoti Jumatatu ijayo Julai 17, 2023.