Home KITAIFA RC SONGWE ATATUA MGOGORO WA SHAMBA LA NAFCO NA WANANCHI MBOZI

RC SONGWE ATATUA MGOGORO WA SHAMBA LA NAFCO NA WANANCHI MBOZI

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Dkt. Francis Michael, ametatua mgogoro wa shamba la NAFCO kati ya wamiliki ambao ni Wakala wa Mbegu ASA na baadhi ya vijiji vinavyozunguka shamba hilo.

Dkt. Michael ametatua mgogoro huo baada ya kufanya ziara katika Kijiji cha Magamba Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe.

Mkuu wa Mkoa huyo amesema alisikia sintofahamu hiyo na akamtuma Mkuu wa Wilaya ya Mbozi Mhe. Ester Mahawe kuangalia hali ilivyo.

“Na sisi kama Viongozi tumeona jinsi tunavyozidi kukaa na kuchelewa kutoa suluhisho la tatizo hili tutakuwa tunawakwaza Wakulima kwasababu ni msimu wa kutayarisha mashamba kwa hiyo kama kuna mgogoro wowote wa ardhi haukupaswa kukalishwa kwa muda mrefu ili tumalize wananchi waendelee na Kilimo”, amesema Rc Dkt. Michael Francis na kuongeza.

“Ndio maana leo nimekuja
ili tuonane na hawa wananchi, migogoro imekuwa mingi ya ardhi lakini tumeitatua naamini na huu umekwisha”, ameeleza kiongozi huyo Mkuu wa Mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe ametoa ekari 500 kutoka katika ekari 1,586 na kuwagawia wananchi wa Vijiji vinne ambapo kila Kijiji kitapewa ekari 125, ambapo awali Vijiji vyote hivyo vilikuwa vikigombea ekari 250.

Amevitaja Vijiji vilivyopewa ekari hizo kuwa ni Magamba, Hangomba, Itewe na Iporoto.

Mkuu wa Mkoa huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuhakikisha maafisa ardhi wanaenda kuhakiki na kupima eneo hilo ili wakulima waendelee na Kilimo.

Akieleza chanzo cha mgogoro huo, Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Mbozi Emmanuel Mamkwe, amesema kuwa ni wamiliki wa shamba la NAFCO kulalamikia mipaka ya vijiji hivyo kuingia katika shamba lao hivyo kuomba Wiraza ya Ardhi kufufua mipaka ya shamba hilo kulingana na ramani ya upimaji iliyopo wizarani mgogoro ambao hata hivyo umefika tamati.

Previous articleWALIOKIRI KUUZA DHAHABU YA BILIONI 346 BILA LESENI KULIPA FIDIA YA SH. MILIONI 924 _ MAGAZETINI LEO IJUMAA NOVEMBA 17/2023
Next articleMAADHIMISHO SIKU YA KISUKARI WANANCHI WAFURIKA MBEYA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here