Husna Hassan,Mtwara
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amewataka waandishi wa habari Mkoa wa Mtwara kuacha kutanguliza mbele maslahi binafsi wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Ameyazungumza hayo leo Novemba 20, 2023 kwenye ukumbi wa Tiffany Diamond wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Habari na Mawasiliano Mkoa wa Mtwara lililoandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambapo kauli mbiu ni yumia vyema kalamu na kamera yako kulinda heshima ya mwanahabari.
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao ya uandishi katika maeneo mbalimbali kupitia kazi za maendeleo katika Mkoa wa Mtwara waache kutanguliza maslahi na badala yake wazingatie misingi,taratibu na maadili ya tasnia hiyo.
“Niwaombe waandishi wahabari kuepuka migongano ya kimaslahi kati yetu na wadau wa habari tunao fanya nao kazi, kuepuka kuandika habari zenye uchochezi na uchonganishi vilevile kuepuka habari za uzushi zenye lengo la maslahi yako binafsi na mnapofanya habari zenu mkumbuke kuwa na usawa kwa kushirikisha angalau pande zote mbili zinazohusika na habari hiyo na mwisho msitangulize mbele maslahi binafsi.”Amesema Abbas
Aidha amewataka pia maafisa habari kwa ngazi ya wilaya na mkoa kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha wanatangaza miradi yote ya mkoa na kimkakati na watoe ushirikiano kwa vyombo vya habari kwa kuwapa taarifa sahihi kuhusu matukio,maelekezo ya mkoa au wilaya pindi yanapohitajika lakini pia kuepuka ubaguzi,upendeleo kwa vyombo vya habari katika matukio ya Mkoa.
Pia amesema mkoa umefikia maamuzi ya kuanzisha jukwaa hilo ili kuwawezesha wanahabari kupata muda wa kujifunza,kujitathimini, kuelimisha na kuhabarisha umma juu ya yale yote yanayofanyika ndani na nje ya mkoa.
Martina Ngulumbi mwandishi wa habari TBC ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuwaaandalia mafunzo hayo kwani yatazidi kuwapa weledi katika utendaji wa kazi na amewaomba wadau wa habari kutoa ushirikiano pindi wanapohitaji kupata usawa wa habari (balabce story) mara baada ya kupata taarifa za awali/malalamiko kutoka kwa chanzo cha taarifa hiyo ili kumrahisishia mwandishi kutoa habari yake kwa wakati.
“Matarajio yangu katika haya mafunzo ni kwamba tumekuwa na changamoto kidogo kwa sisi waandishi wa habari kutopata ushirikiano wa kutosha wakati wa kutaka kupata usawa wa taarifa(balance story) unakuta mwandishi anaenda field anarudi anamfata kiongozi wa taasisi au kiongozi wa shirik
a flani ili kupata usawa wa taarifa (balance story) yake kunakuwa na ugumu flani hivyo unakuta hiyo habari Baada ya kuipeleka siku hiyo mtu anailaza anaipeleka siku ya pili au wakati mwengine unakuta unaiacha kabisa kwasababu huwezi kutoa taarifa ambayo haija kamilika hivyo kupitia haya mafunzo naamini kwa kua tupo na viongozi wa serikali maafisa habari wa mkoa,wa taasisi na halmashauri zote tisa nina amini hizo changamoto zitabaki kuwa historia kwasababu tupo nao kwenye mafunzo ndani ya hizi siku 4.”Amesema Martina
Kwa upande wake Bryson Mshana Katibu wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Mtwara amesema uzinduzi wa jukwaa hili la habari na mawasiliano ni moja ya hatua kubwa kwenye sekta ya habari ndani ya mkoa na amewaomba wadau kuendelea kuunga mkono katika kuboresha sekta hiyo.
“Uzinduzi huu ni moja ya hatua kubwa kupigwa katika sekta ya habari ndani ya mkoa wetu huu wa Mtwara kwasababu ni kitu ambacho tulikuwa tunakihitaji muda mrefu kwaajili ya kuwaunganisha wanahabari na wadau wengine wa sekta ya habari hivyo ni jambo zuri na nafikiri ni historia sidhani kama kwa mikoa mingine ina jukwaa kama hili na kama ipo sio kwa ukubwa huu sisi tumefanya kitu ambacho kitaenda kuwa mfano kwa mikoa mingine na jukwaa kama tulivyosikia ni endelevu litafanywa kila mwaka na tutakuwa tunazunguka wilaya mbalimbali ndani ya mkoa wa Mtwara.”Amesema Mshana