Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda amewataka watalamu wa afya mkoani Songwe kutumia vizuri huduma ya usafirishaji wa dharura kwa akina mama wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga ambao unafaamika kwa jina la M-MAMA kwa kudhibiti vifo ambavyo vinatokana na changamoto ya ukosefu wa usafiri kwa akina mama wajawazito na watoto.
Katibu Tawala, Bi. Happiness Seneda ametoa wito huo wakati akifungua rasmi huduma ya M-MAMA pamoja na kituo cha mawasiliano kitakachokua kinaratibu huduma zote za usafirishaji wa dharua kilichopo Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Songwe.
Bi. Happiness Seneda amesema kwa sasa huduma ya usafiri ya dharura sio changamoto tena kwa akina mama wajawazito na haipaswi kuwa chanzo cha vifo kwa akina mama na watoto, ni wajibu wetu kuitumia vizuri huduma hii.
Pia, Katibu Tawala, Bi. Happiness Seneda amewataka watalamu wa afya kwa sasa kujiikita zaidi katika ukusanyaji wa damu salama ili pale mama anapokuwa na changamoto ya damu anapatiwa haraka.
Mratibu wa M-MAMA Mkoa wa Songwe, Gladyness Richard amesema huduma ya M-MAMA watatumia watalamu wa afya kwenye vituo vya kutolea huduma pale ambapo watapata mama mjamzito, mtoto au mama aliyejifungua aliyepata changamoto za kiafya na anahitaji huduma ya rufaa kwenda Kituo cha huduma za Afya.
Hadi sasa tayari tuna madereva wapatao 74 ambao wamesajiliwa kusaidia katika usafirishaji wa dharura ambao wameunganishwa na Mfumo na pale tu mgonjwa atakapokuwa kwenye kituo basi mtalamu akipiga simu kwenye kituo chetu cha mawasiliano ataangalia ni dereva gani yuko jirani na kituo hicho kwa wakati huo, amesema Mratibu wa M-MAMA Mkoa wa Songwe, Gladyness Richard.
Meneja wa Vodacom Mkoa wa Songwe, amesema wao kama wawezesha wa Mfumo wa M-MAMA wameimarisha mfumo wa mawasiliano na mtandao ili kusitokea changamoto yeyote pale tu huduma ya usafiri wa dharura inapohitajika..