Rais wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ameagiza vibali vya minara iliyosainiwa leo visizidi zaidi ya mwezi mmoja viwe vimetoka.
Rais Samia amesema hayo katika hafla ya utiaji saini Mikataba ya miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano ya Simu katika kata 763 nchini ambapo amewaonya viongozi wanaochelewesha.
“Wale wenye makoti mazito ambayo hayainui mikono wakati wa kusaini naomba makoti yavuliwe ili yawekwe kwenye kiti ili watoe vibali kisheria kwa kufuata kanuni tulizojiwekea”
Amesema kumekuwepo na urasimu katika utoaji wa vibali “nlikuwa nazungumza na wizara wakaniambia ili mnara usimame unachukua hata miezi sita kupata kibali kutoka kwa taasisi husika sasa tutaitana na wale wote wanaohusika na mambo ya utoaji wa vibali”
Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha huduma bora za mawasiliano zinawanufaisha wakulima hasa katika shughuli zao za kilimo kupitia maboresho yanayofanywa na serikali kwa kupeleka mawasiliano vijijini.
“Kuwepo kwa huduma bora za mawasiliano hususani katika maeneo ya vijijini ni muhimu sana kiuchumi, kisiasa, kijamii lakini hata kiutamaduni lakini hata katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi yetu.” amesisitiza