
Siku ya Ushairi wa Watoto Duniani (WoChiPoDa-World Children’s Poetry Day imeadhimishwa Oktoba 07, 2023 katika shule ya msingi Mkoani na shule ya msingi Kambarage zilizopo wilaya ya Kibaha mkoani Pwani ambapo dhima ya mwaka huu ikiwa ni mimea
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mratibu wa WoChiPoDa Mkoa wa Pwani Bi. Rehema Kawambwa amesema, lengo la siku hiyo ni kuimarisha ari na morali kwa watoto kupenda kutunga na kuandika mashairi pamoja na kuwajengea watoto hamasa ya kupenda kusoma vitabu.
“Siku hii inatukumbusha wazazi, walezi na walimu kuwahamasisha watoto wetu, kuamsha ari zao na kuwapa motisha zaidi katika kupenda kuandika na kusoma vitabu, kutunga na kughani mashairi” alisema Bi. Kawambwa

Siku hii huadhimishwa kila Jumamosi ya kwanza ya mwezi Oktoba kila mwaka na ilianzishwa mwaka 2014 na Bi. Gloria Gonsalves aishiye nchini Ujerumani lengo likiwa ni kuwapa watoto motisha, ari na morali ya kupenda kuandika, na kuwajaza upendo katika usomaji wa mashairi ili kuwajengea mazingira mazuri katika kujifunza mambo mbalimbali yanayowazunguka kwenye jamii zao kupitia uandishi, na usomaji wa mashairi na vitabu kwa ujumla.