NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Wakili wa kujitegemea Boniface Mwabukusi amefika mbele ya Jeshi la Polisi makao makuu Mkoa wa Mbeya na kuhojiwa juu ya tuhuma za kufanya kusanyiko lisilo halali huko Busokelo wilayani Rungwe mwishoni mwa juma lililopita.
Wakili Mwabukusi amekiambia kituo hiki kuwa aliitwa na Polisi jana (Oktoba 09, 2023) lakini aliahidi kwenda leo (Oktoba 10, 2023) ambapo amehojiwa na kutoa maelezo yake kuhusu kufanya kusanyiko lisilo halali.
Amesema alipofika polisi aliandika taarifa zake binafsi na hakuna taarifa zozote alizotoa zaidi.
“Aaah nilipofika asubuhi pale polisi niliandika particulars zangu (taarifa binafsi) kwa maana ya majina na vitu vingine binasfi lakini kuhusu madai yao nimewaambia kisheria nitayatoa tutakapofika mahakamani. Hata jioni nilipoitwa tena yalikuwa ni yaleyale”, Ameeleza wakili Mwabukusi.
Aidha wakili Boniface Mwabukusi amesema baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa na jeshi la polisi aliachiwa kwenda kuendelea na majukumu yake hadi baadaye baada ya majuma mawili ambapo ataripoti polisi.
Naye wakili wa kujitegemea Philip Mwakilima amesema Balozi mstaafu Dkt. Wilbroad Slaa pamoja na mwenyekiti mtendaji wa mtandao wa TRAFO Buberwa Kaiza ambao walishikiliwa tangu jana Oktoba 09, 2023 nao wakihusishwa na tuhuma za kufanya mkutano usio halali walihojiwa na kumaliza mahojiano yao majira ya saa moja usiku wa jana (Okt.09, 2023).
Wakili Mwakilima anasema pia Buberwa na Dkt. Slaa watatakiwa kuripoti polisi baada ya majuma mawili huku taarifa kuhusuwanaharakati Mdude Mpaluka Nyagali zikidai kuwa hajaenda polisi tangu alipoitwa Oktoba 09, 2023 akidaiwa kuhusishwa kwenye tuhuma hizo.
Wakati hayo yakiendelea Mdude ambaye ni mratibu wa maandamano ya amani ya kupingakataba wa bandari na kudai katiba mpya Mdude Nyagali Mpaluka amesisitiza kupitia waraka wake hivi karibuni azma ya kuendelea kuratibu maandamano hayo anayodai yatazinduliwa jijini Mbeya Novemba 09, 2023.