Tume ya Taifa ya umwangiliaji kwa mwaka wa fedha 2023/24 imepanga kutekeleza jumla ya miradi 822, ambapo miradi 114 ni ya ujenzi wa mabwawa na 103 ni ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa tume ya Taifa ya umwagiliaji, Raymond Mndolwa wakati akitoa taarifa Kuhusu Utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Umwagiliaji na mwelekeo wake Kwa mwaka wa fedha 2023/24 Katika Ukumbi wa idara ya habari – Maelezo julai 29, 2023 jijini Dodoma.
Mndolwa amesema Mabwawa hayo yatawasaidia Wakulima kuweza kulima Zaidi ya vipindi viwili kwa mwaka bila changamoto yoyote kwa kuwa mabwawa hayo yatakuwa bora nayauhakika huku akisisitiza kilimo hicho kitakuwa ni kilimo chenye tija nakitachangia kukuza uchumi katika jamii na taifa kwa ujumla.
Amesema katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, mwelekeo wa Tume ni kuendelea kutekeleza miradi itakayoongeza eneo la umwagiliaji lenye ukubwa hekta 256,185.46 ili kufikia hekta milioni 1,200,000 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020).
“Katika mwaka huu wa Fedha tutakarabati miundombinu ya umwagiliaji katika Skimu 24 zenye jumla ya hekta 32,092; kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa mabwawa mapya 100 yenye wastani wa mita za ujazo 936,535,700 na kuanza ujenzi wa mabwawa hayo,”amesema Mndolwa.
Pia Tume hiyo itakamilisha ujenzi wa mabwawa 14 yenye mita za ujazo 131,535,000 yaliyoanza kujengwa Mwaka 2022/2023, kukamilisha usanifu wa mabonde 22 ya Umwagiliaji ulioanza Mwaka 2022/2023.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa tume hiyo pia imejipanga kutumia Teknolojia katika kuhakikisha wanaboresha upatikanaji wa Maji na kuwasaidia wakulima kuwa na uhakika wa Maji Kwa misimu yote.
Mndolwa ametoa wito Kwa wakulima kulipa ada ili kuendelea kuboresha Mazingira ya kilimo Cha umwagiliaji hapa Nchini.
“Nitumie Fursa hii kuwaomba wakulima kulipa ada wachangie maendeleo ya Tume ili tuweze kuwahudumia Kwa uhakika,”amesema Mndolwa.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa tume hiyo itaanza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mabonde 22 yenye jumla ya hekta 306,361, kuanza ujenzi wa skimu mpya 35 zenye jumla ya hekta 111,390.