Na Theophilida Felician Kagera.
Ndege yenye namba za usajili 9127 Mali ya Jeshi la wananchi Tanzania JWTZ imepata ajali na kuanguka maeneo ya uwanja wa ndege Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera.
Akizungumzia juu ya kutokea kwa ajali ya ndege hiyo kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Kagera ACP BLASIUS Z, CHATANDA amesema kuwa tukio hilo limetokea hii leo tarehe 20 Julai mwaka 2023 mnamo majira ya saa tatu na nusu 3:30 asubuhi.
Kamanda Chatanda amefafanua kuwa ndege hiyo ilikuwa katika mafunzo yanayoendelea ambapo ndani yake walikuwemo marubani wawili ambao ni Meja Renadi Revokatus Mkundwa Muha mwenye umri wa miaka (45) pamoja naye Luteni Alex Venance Moshi Mchaga umri miaka 30.
Amesema kuwa watu hao wawili wamepelekwa Hosptalini na kufanyiwa uchunguzi kiafya hivyo wamebainika kuwa salama na kuruhusiwa.
Hata hivyo ameongeza kuwa chanzo cha ajali ya ndege hiyo hakikufahamika mara moja na uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha ajari hiyo.
Mkuu wa wilaya Bukoba Erasto Sima amewashukuru jeshi la zima Moto na uokoaji pamoja na wadau wengine waliojitokeza na kuwahi kufika eneo la tukio mapema hatimaye kusaidia kuwaokoa marubani hao.