Home KITAIFA NCHIMBI AANZA NA MAMBO MATATU, AKIPOKELEWA ZANZIBAR

NCHIMBI AANZA NA MAMBO MATATU, AKIPOKELEWA ZANZIBAR

Akemea makundi ya uchaguzi, aweka msimamo serikali ya Umoja wa Kitaifa na chama kusimamia serikali

Mapokezi makubwa yamsubiria Dar es Salaam, Januari 20, 2024.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amekemea na kuonya tabia ya baadhi ya wanaCCM wanaovunja taratibu za chama kwa kuendekeza makundi baada ya uchaguzi, akisema haikubaliki na haitavumiliwa ndani ya CCM.

Amesema kuwa ni muhimu kiongozi anayeshinda awe mnyenyekevu kutumikia nafasi yake aliyochaguliwa na yule anayeshindwa anapaswa kuvumilia hadi mwaka mwingine, huku akisisitiza kwamba mambo yote mawili, kushinda na kushindwa katika uchaguzi, huenda sambamba na mipango ya Mungu.

Ndugu Dkt. Nchimbi amesema hayo wakati akiwahutubia wanachama wa CCM na wananchi wa Zanzibar, waliojitokeza kwa wingi wakati wa mapokezi ya kumpokea kiongozi huyo, yaliyofanyika leo Ijumaa, Januari 19, 2024 ofisi kuu ya CCM Zanzibar, iliyoko eneo la Kisiwandui, Unguja.

Aidha, Ndugu Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kimedhamiria kwa dhati kuyaenzi mapinduzi matukufu ya Zanzibar na kuhakikisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, inadumishwa ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuwaenzi waasisi wa mapinduzi hayo, ambao walikusudia kuhakikisha Wazanzibar wote wanakuwa wamoja katika kutafuta ustawi na maendeleo ya Zanzibar, bila kujali tofauti za kisiasa, kidini, rangi, kabila, wala hali zao za maisha.

“Wana-CCM wote tunapokwenda kwenye uchaguzi tutaanza kumnong’ononeza mtu mmoja unataka kugombea anakwambia anakuunga mkono anakuwa wa kwanza, unamnong’oneza wa pili, wa tatu, wa nne wakati mwingine wanafika 20,30,40 wakishafika hapo wanaitwa kundi kwa hiyo unakuwa na kundi lako wewe na wenzako, hivyo hivyo na mwingine na mwingine hivyo. Tukimaliza uchaguzi makundi lazima yafe. Unapotaka kupika ndiyo unawasha moto, ukiipua unauzima moto wako. Ni mjinga peke yake anayekoleza moto wakati kishapakua.

“Kwa hiyo nawasihi wana CCM habari za uchaguzi lazima ziishe, walioshinda lazima wawe wanyenyekevu na walioshindwa lazima wajue kushindwa au kushinda kuko katika mapenzi ya Mwenyezi Mungu utashindwa leo, utashinda kesho. Mimi nimegombea nadhani mara 27 nimeshindwa mara sita na wala haikuwa shida. Ukiamua kuwa mwanasiasa kushindwa nayo raha, kwanza ukiwa mwana siasa hujawahi kushindwa wewe siyo mwanasiasa,” amesema Ndugu Dkt. Nchimbi.

Previous articleKIONGOZI WA KANISA AZUIA WANAFUNZI KWENDA SHULE KWA MADAI YESU ANARUDI, SERIKALI YAINGILIA KATI- MAGAZETINI LEO IJUMAA JANUARI 19/2024
Next articleBASHE ATAJA SABABU UPUNGUFU WA SUKARI, TANI 100,000 ZAAGIZWA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here