Home KITAIFA NAIBU WAZIRI NDERIANANGA ATETA NA WANAFUNZI WA WERUWERU

NAIBU WAZIRI NDERIANANGA ATETA NA WANAFUNZI WA WERUWERU

Na. Mwandishi Wetu- Moshi

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe.Ummy Nderiananga awaasa vijana kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili kuyafikia malengo waliyonayo.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Weruweru alipotembelea mapema Julai 16, 2023 shuleni hapo kwa lengo la kuwapa hamasa wanafunzi wa shule hiyo ambayo aliwahi kusoma na kutoa zawadi za taulo za kike na mafuta ya ngozi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi ikiwa ni sehemu ya shukrani kwa uongozi wa shule hiyo.

Mhe. Nderiananga aliwaeleza upo umuhimu wa kuendelea kuchukua tahadhari za masuala yanayohusu Virusi vya UKIMWI kwani kwa mujibu wa tafiti za viashiria vya VVU na UKIMIWI mwaka 2016/17 zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya maambukizi ipo kwa vijana mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 hivyo ipo haja ya kuendelea kuwa makini.

Alitumia fursa hiyo kuwahimiza kujikinga na mimba za utotoni na kutokatishwa tamaa juu ya ndoto zao.

“Katika maisha kukatishwa tamaa kupo, lakini kuwa imara hadi wakatisha tamaa wakate tamaa wenyewe, hivyo wanafunzi wa Weruweru muwe imara, majasiri na hakika jitihada zenu hazitapotea bure,” alisema

Sambamba na hilo aliwatoa wasiwasi wanafunzi wa kidato cha sita kuhusu kuendelea na elimu ya juu kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga bajeti ya kutosha katika sekta ya elimu kwa ajili ya kuwawezesha mikopo ya Elimu ya juu.

“Jukumu lenu kubwa ni kuongeza bidii, nidhamu na weledi katika masomo yenu ili kupata fursa ya kuendelea na masoma ya elimu ya juu kisha kuzifikia ndoto mlizo nazo,” alisisitiza Mhe Nderiananga

Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mwitikio wa Taifa TACAIDS Bi.Audrey Ngelekela aliwakumbusha kuendelea kuwa makini kujiepusha na mitandao ya ngono pamoja na kuchukua tahadhari ili kujiepusha na maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Alieleza kuwa, Serikali kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa jamii hasa vijana ambao ndio kundi linaloathiriwa zaidi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa mwaka 2016/17.

Naye Mratibu wa UKIMWI wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Dkt. Didas Constantine aliwakumbusha wanafunzi umuhimu wa kupima afya zao kwa lengo la kujua hali zao za maambukizi iwapo unagundulika kuwa maambukizi inashauriwa kuanza dawa mapema.

Awali akizungumza kuhusu shule ya Weruweru mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi.Rozalia Frimin alimshukuru Naibu waziri kwa ziara yake shule hapo pamoja na kuwapa zawadi ya taulo za kike pamoja na mafuta kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi ikiwa ni sehemu ya shukrani yake kwa mchango wa shule hiyo katika maisha yake.

“Mhe Naibu Waziri tunakushukuru kututembelea leo, hii imetupa hamasa zaidi sisi na wanafunzi wetu kwa kuwa umetambua mchango wa shule ya Weruweru, sisi tutaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuzalisha vijana wasomi na wenye maadili mazuri nchini,” alisema Mwalimu Frimin.

Previous articleJINSI NILIVYOSHINDA MILIONI 20 ZA BAHATI NASIBU KWA URAHISI
Next articleSIMBA ALIYEKUWA ANAKULA MIFUGO IRINGA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here