NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Jimbo la Mbeya vijijini kimetangaza kumfutia uanachama Joseph Mwasote (China wa China) ambaye ni Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa wa Mbeya akidaiwa kuwa chanzo cha migogoro ndani ya Chama hicho.
Akitangaza maazimio ya Kamati tendaji ya Chadema Mbeya vijijini Mwenyekiti wa jimbo hilo Jackson Mwasenga amesema mwanachama wake Joseph Mwasote ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Mbeya na makamu Mwenyekiti Kanda ya Nyasa amesema kiongozi huyo amekuwa chanzo cha migogoro ndani na nje ya jimbo hilo.
Viongozi hao wanasema wamemwita mara kadhaa kiongozi huyo lakini hakuitikia wito na kwambabamekuwa akizunguka kwenye kata mbalimbali kupanga timu ya kuwapindua viongozi wa jimbo.
“Haijalishi tumekosea au hatujakosea lakini Kamati tendaji ya Jimbo (Mbeya vijijini) kwa pamoja tumeazimia kumfutia uanachama Joseph Mwasote. Migogoro mingi chanzo ni yeye, kwenye kata huko anazunguka kwa nia yake binafsi anaunda kakikundi kaje katuondoe sisi (Jimbo), hata kupita ofisini kuja kusaini akiwa anaenda huko katani hataki sasa huu sio utaratibu”, Jackson Mwasenga, Mkiti CHADEMA Mbeya vijijini.
Hata hivyo bado wako wanachama wanaodaiwa kukamatwa kwa saa kadhaa na polisi wakidaiwa kutaka kuandamana kwenye ofisi ya jimbo mjini Mbalizi walipofika kutaka kujua hatma ya mwenyekiti wao kuondolewa.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo Joseph Mwasote mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Mbeya ameeleza kusikitishwa na maamuzi ya jimbo akisema mamlaka yake ya nidhamu iko ngazi ya tawi analotoka na ngazi ya kanda ambako pia ni kiongozi huku akisema hana barua ya kusimamishwa uanachama wake.
Kuhusu kuwa chanzo cha migogoro Mbeya vijijini na maeneo mengine ikiwemo Mbeya mjini amesema ni maneno ya maslahi binafsi ya viongozi wa Mbeya vijijini na kutoa ole kwa viongozi na wanachama wanaoendelea kukichezea chama hicho anachodai ni tegemeo na mkombozi wa Watanzania.
“Lakini wameikosea Katiba sana (ya CHADEMA). Anayeshikilia uanachama wangu ni Tawi (Isanga-Imezu), anayeshikilia uanachama wangu ni mamlaka yangu ya nidhamu ngazi ya juu. Yaani leo mkuu wa Wilaya akamuondoe Mkuu wa Mkoa! ni shida”, Joseph Mwasote (China), Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya baada ya kufutiwa uanachama na Jimbo lake la Mbeya vijijini.
Kwa miaka ya hivi karibuni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoani Mbeya kimekuwa kikihusishwa na migogoro ya ndani mara kwa mara hali ambayo inaharibu taswira na nia ya Chama kwa wafuasi wake ambapo sababu mbalimbali zimekuwa zikitajwa ikiwemo uchu wa madaraka, kushindwa kutii itifaki ndani ya Chama na kutofuata hatua za ndani ya Chadema kunapokuwa tatizo.