Home KITAIFA MTUMISHI MBOZI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UHUJUMU UCHUMI

MTUMISHI MBOZI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UHUJUMU UCHUMI

NA JOSEA SINKALA, SONGWE.

Aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa kituo cha afya Iyula Halmashauri ya Mbozi mkoani Songwe Eunice Mkoni, amefikishwa mahakamani mkoani Songwe na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe, akituhumiwa kwa makosa manne ya udanganyifu na uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa TAKUKURU Mkoani Songwe, mshtakiwa anatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha shilingi  37,811,720/= pamoja na makosa mengine ya kumdanganya mwajiri kwa manufaa yake binafsi.

Ubadhirifu huo unaelezwa kuwa kinyume na kifungu namba 28 (1) na (3) cha Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa sura ya 329 kilichofanyiwa marekebisho mwaka wa jana (2022) na kifungu namba 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 na marejeo ya mwaka 2022.

Pia mshtakiwa anatuhumiwa kwa madai ya matumizi ya nyaraka kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu namba 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 kilichorekebishwa mwaka 2022 pamoja na matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2022.

Hata hivyo Mshtakiwa Eunice Mkoni amekana makosa yote manne ambapo ameendelea kusalia Rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na shauri hilo namba 07/2023 limeahirishwa na Mahakama mkoani Songwe hadi terehe nyingine kwa ajili ya kuanza usikilizwaji hoja za awali.

Previous articleVIFAA VYA KISASA VYAPELEKEA WANAWAKE KUOMBA KUJIFUNGUA VYA OPARESHENI
Next articleICE CREAM ZA AZAM ZAYEYUSHWA JANGWANI.. KIKWETE , KINANA WATOA SIKU 14_ MAGAZETINI LEO ALHAMISI AGOSTI 10/2023

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here