Wakati Serikali,wanaharakati na viongozi wa dini wakiendelea kukemea vitendo vya ukatili katika Jamii,Mtoto wa miaka 6, leonila John Maletu, mkazi wa kijiji cha Kibosho Sinde , Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro amebakwa na kulawitiwa na kisha kuuawa na mwili wake kutupwa kwenye korongo.
Mtoto huyo ambaye ni Mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Msingi Wereni iliyopo katika kijiji hicho, alikutwa na mkasa huo siku ya Mei 31 mwaka huu wakati alipokuwa akienda ‘tuition’ masomo ya ziada baada ya shule kufungwa.
Inadaiwa kuwa, siku hiyo mwanafunzi huyo baada ya kuondoka nyumbani kwa wazazi wake akiwa mwenyewe kama ilivyo kawaida yake hakufika katika vipindi vyake vya ziada (tuition) siku hiyo ambapo Mwalimu aliyekuwa akimfundisha alipiga simu nyumbani kwa wazazi kuwa Mwanafunzi huyo haonekani na amechelewa kufika shuleni.
Baada ya wazazi wa Mwanafunzi huyo kupigiwa simu na mwalimu, ilipigwa mbiu kijijini hapo kumtafuta mtoto huyo na hakuonekana na ndipo wazazi walienda kutoa taarifa kituo cha polisi ambapo kesho yake Juni Mosi mwanafunzi huyo mwili wake ulikutwa umetelekezwa eneo la korongo huku mwili wake ukiwa hauna nguo na akiwa anavuja damu sehemu za siri.
Katika eneo hilo zilikutwa nguo za mtoto huyo pamoja na nguo ya ndani ya mwanaume(boxer) jambo ambalo lilizua taharuki kubwa baada ya kijana mmoja ambaye ni dereva bodaboda kwenda kutoa taarifa ya kuonekana kwa mwili wa mtoto huyo ambapo kijana huyo baadaye alipokamatwa na kukaguliwa alikutwa hajavaa nguo ya ndani jambo ambalo lilizua taharuki kubwa.
Mama mzazi wa mtoto huyo baada ya kushuhudia tukio hilo alipoteza fahamu na mpaka sasa amelezwa katika kituo cha afya Umbwe akipatiwa matibabu kutokana na mshituko alioupata.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo alisema tukio hilo lilitokea Mei 31, mwaka huu na kwamba wanashikiliwa watu kadhaa kuhusiana na mauaji ya mtoto huyo.
“Hili tukio ni kweli limetokea na huyu mtoto amebakwa na kulawitiwa na amefariki, lakini kwa sasa tukio lipo kwenye uchunguzi zaidi, hili tukio tunalifuatilia kwa ukaribu sana lakini tunaomba ushirikiano kwa wananchi na tumejipanga kwenda kuongea na wananchi wa lile eneo,”alisema Kamanda Mdogo.
“Kwasasa bado tunaendelea na uchunguzi wa kina na tumefikia sehemu nzuri na wapo baadhi ya watu tunawashikilia, upelelezi ukishakamilka tutachukua hatua nyingine za kisheria,”alisema Kamanda Mdogo.
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa wasaidizi wa kisheria pamoja na jirani wa familia hiyo, Vicky Massawe alisema tukio hilo limezua taharuki kutokana na mauaji hayo ya kikatili ambayo yamefanyika katika kijiji hicho.
“Mtoto alikuwa anakwenda ‘tuition’ na sio mbali sana na nyumbani kwao, lakini kuna sehemu mara nyingi anapenda kucheza na wenzake, sasa hiyo siku hakwenda ‘tuition’ kwa hivyo ikabidi wazazi wapigiwe simu kwanini mtoto hajafika ,”
“Baada ya wazazi kupigiwa simu kwamba mtoto hajafika ‘tuition’ na muda ulikuwa umepita, wazazi pamoja na viongozi wa kijiji walipiga mbiu kumtafuta mtoto maana na nyumbani nako hakuonekana, mpaka asubuhi kuna kucha mtoto hakupatikana,”
Alisema ilipofika Juni Mosi, muda wa saa mbili asubuhi zilipatikana taarifa kutoka kwa dereva bodaboda kwamba kuna mwili wa mtoto umeoenekana kwenye eneo hilo la korongo ambapo mdomo wa mtoto huyo ulikuwa umefungwa na nguo huku sehemu ya shingoni kukiwa kumefungwa na sweta.
“Kutokana na mazingira ya tukio, alihojiwa yule boda boda kwamba amemwonaje huyo mtoto kwenye korongo akasema kuna mtu alikuwa kwenye hilo eneo anachuma mapera ndiye akawa amemwona huyo mtoto na ndiye aliyempa taarifa, lakini cha kushangaza katika lile eneo hakuna mti wenye mapera ya kuchuma na ilikuwa ni asubuhi sana,”
“Wananchi karibu kijiji kizima wakaitana asubuhi ile wakaenda kwenye eneo ambalo wanasema mtoto ameonekana, mtoto alikuwa amefungwa mdomo na nguo zake ziko pembeni na katika kuangalia zile nguo za huyo mtoto kulikuwa na ‘boksa’ ya kiume tukawa tunajiuliza hiyo boksa ni ya nani ,”
Alisema tukio la kushangaza zaidi dereva boda boda aliyepelekea taarifa wa kwanza ya kwamba ameuona mwili wa mtoto huyo , alipotafutwa na kukamatwa alikutwa hajavaa boksa na hapo awali eneo la tukio mwili wa mtoto ulipokutwa kulikuwa na boksa pamoja nguo za mtoto huyo.
Akizungumzia tukio hilo , Mwenyekiti wa kijiji jirani, Umbwe kati, Michael Mushi, alisema eneo ambalo tukio hilo limetokea ni eneo hatarishi sana kwa kuwa kuna wavutaji bangi, wauza gongo pamoja na wala mirungi ambapo alisema tukio hilo ni hatari sana.
“Katika maeneo hayo matukio ya ubakaji kwa watoto ni mengi kutokana na kwamba watu hawapo tayari kutoa ushirikiano pindi matatizo kama hayo yanapojitokeza na kwamba hata kwenye mikutano ya kijiji watu wamekuwa hawashiriki” alisema Mushi
Aliongeza kuwa “Kwa kweli hili tukio lililotokea hapa kijiji jirani ni tukio baya sana na linaumiza mno, huyu mtoto ameuliwa kikatili sana, tuseme ni unyama wa hali ya juu, haupaswi kufanywa na binadamu kwa kweli,”alisema Mwenyekiti huyo.