Msemaji Mkuu na Mkurugenzi wa idara ya habari Maelezo Gerson Msigwa ameiasa jamii kujenga tabia ya kwenda kupata huduma katika vituo vya afya na kuacha dhana ya kukimbilia kwa wataalam wa tiba asili hali inayopelelekea kupoteza muda bila uponyaji na kutumia gharama kubwa.
Msigwa ameyasema hayo Agosti 3, 2023 jijini Dodoma wakati wa Mkutano kati ya waandishi wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya mifupa na ubongo Muhimbili (MOI).
“Kuna baadhi ya watu wakiwa wagonjwa badala ya kwenda kwenye vituo vya afya wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji na huko hawapati tiba stahiki, na kuchelewa kupata matibabu na wengine wanapoteza maisha na baadhi wanatapeliwa kwa kutoa gharama kubwa za kulipia huduma hizo ihali Serikali imewekeza katika vituo vya afya”.
Msigwa ameendele kuwataka wahusika wanaotoa huduma ya tiba mbadala wafuate utaratibu uliopangwa ili kuepuka athari zinazowapata wananchi pale wanapofuata tiba hizo.