SERIKALI kupitia Bohari ya dawa (MSD) Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 imetenga Shilingi bilioni 205 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya.
Hayo yamesemwa na Meneja mipango, ufuatiliaji wa tathmini wa bohari ya dawa (MSD) Hassan Ibrahim wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Bohari hiyo na nwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24 Agosti 7,2023 jijini Dodoma.
Ibrahim amesema Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa (MSD) takriban miaka 30 iliyopita Serikali katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 imeipatia Bohari ya Dawa Shilingi bilioni 157.56 kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa.
“Ununuzi wa bidhaa za afya unafanyika kwa kufuata Sheria za Ununuzi wa Umma na Kanuni zake ikiwa ni pamoja na kutumia mifumo ya TEHAMA iliyowekwa na Serikali na ile ya ndani ili kuchochea ufanisi,”.
Pamoja na hayo amesema MSD imejipanga Kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na miundombinu ya utunzaji wake ambapo ujenzi wa maghala unatarajiwa kuanza mwezi Agosti 2023.
“Katika kuendana na kasi ya ongezeko la vituo vya afya inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita, Bohari ya Dawa imekuwa ikifanya mawasiliano na balozi zetu zilizopo China, Algeria, Korea ya Kusini, Urusi na maeneo mengine duniani ili kuweza kufanya utambuzi wa wazalishaji, wawekezaji na kuwezesha ununuzi wa bidhaa za afya kwa uhakika, ubora na gharama nafuu,” amesema Ibrahim.
Hata hivyo amesema MSD ipo kwenye maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa na bidhaa za pamba tiba.
“Kujenga maghala ya kisasa katika mikoa ya Dodoma, Mtwara na Kagera kwa lengo la kuongeza nafasi za kuhifadhi bidhaa na kuimarisha ubora wa bidhaa za afya,” ameongeza kwa kusema Ibrahim.
Bohari ya Dawa (MSD) ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya na majukumu yake ni Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo vya afya vya umma na binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Mwishooo…