

Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imelenga kuhakikisha inaiunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami jitihada ambazo zinajidhihirisha kwa uwepo wa miradi mingi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ndani ya mkoa husika ili lengo hilo litimie na hatimaye kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji ili kuchangia uchumi wa mkoa husika na taifa kwa ujumla.
Mkoa wa Kigoma ni Mkoa ambao kwa asilimia chache bado haujanganishwa kwa barabara na mikoa jirani pamoja na mikoa mingine nchini lakini kwa uwepo wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa kwa kasi ndani ya mkoa huu, inaashiria kwamba ndani ya muda mchache sana kutoka sasa Mkoa wa Kigoma utakuwa umeshaunganishwa kwa miundombinu ya barabara.
Malengo na jitihada hizi, haziendi mbali na kauli za Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe akiongea na waandishi wa habari wakati wa kutembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Maragarasi-Ilunde-Uvinza yenye urefu wa 51.1 kwa kiwango cha lami ambapo amesema mradi huo umefikia asilimia 31 ya utekelezaji wake.
Mhandisi Mirumbe ameongeza kuwa, mradi wa Maragarasi-Ilunde-Uvinza ni sehemu ya barabara kutoka Kigoma-Uvinza-Maragarasi yenye urefu wa 212.
“Mradi wa Uvinza-Malagarasi (KM 51.1) ambao ni sehemu ya barabara kutoka Kigoma-Uvinza-Malagarasi ambao ni kilometa 212 huku kilometa 105 kutoka Kigoma hadi Uvinza zikiwa zimeshajengwa kwa kiwango lami tayari ambapo sasa hadi kuelekea Tabora zimesalia Kilometa 61 ambazo zote mkandarasi yuko site akiendelea na kazi” alisema Mhandisi Mirumbe

Kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Mirumbe ameeleza kuwa unatarajiwa kukamilika tarehe 7 Oktoba, mwaka huu
Kuhusu manufaa ya mradi kwa jamii, kaimu meneja huyo amebainishi kuwa, mradi umeajiri wafanyakazi 216 kati yao wafanyakazi wageni wakiwa ni 21 pekee.
Kwa upande wake Kaimu Mhandisi Mkazi, Mhandisi Yusuf Karera amesema, hadi sasa kazi mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo zimefanyika ikiwemo kujenga makaravati 22 huku makaravati madogo yakiwa ni 19 na makaravati matatu.

Mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Maragarasi-Ilunde-Uvinza yenye urefu wa 51.1 unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 62. Mradi huu unatekelezwa kupitia mkandarasi STECOL Cooperation chini ya mhandisi mshauri Norplan Tanzania Ltd.