Na Joel Maduka, Geita
Kufuatia kundi la vijana kuonekana kuwa sehemu ya kuathirika na machafuko ya kukosekana kwa amani, shirika lisilo kuwa la kiserikali la Himiza Social Justice kupitia mradi wa mtandao wa vijana wa nchi tano za maziwa makuu ,ambao unatekeleza mradi kwa mikoa minne,Mwanza,Kigoma,Geita na Kagera wamewakutanisha vijana kwaajili ya kuwajengea uwezo wa kujua namna gani wanaweza kuwa watetezi wa Amani.
Mratibu wa mradi wa Taifa wa nchi za maziwa makuu Jimmy Luhende amesema wamekutana na vijana Mkoani Geita kwa nia ya kuwaelezea na kuwafundisha juu ya faida za kulinda Amani na utulivu kutokana na vijana wengi kuwa ndio wamekuwa wakiathirika na machafuko ambayo yamekuwa yakijitokeza na kupelekea uchafunzi wa Amani kwa Nchi ambazo zipo kwenye maziwa makuu.
“Mradi wa Nchi za maziwa makuu unatekelezwa kwenye Nchi tano ambazo ni Uganda ,Rwanda,Congo ,Burundi na Tanzania tunawashirikisha zaidi ya vijana 120 ambao wanapata mafunzo mbali mbali ya kulinda na kutunza Amani na kwa Nchi yetu tuna Mikoa minne kwa maana ya Mwanza,Geita,Kagera na Kigoma nia yetu ni kuona wanapata uwezo wa kujua njia zilizo nzuri za kutunza amani ambayo ndio chachu ya maendeleo na utulivu kwa Nchi”Jimmy Luhende Mratibu wa mradi wa Taifa wa nchi za maziwa makuu.
Jimmy ameongeza kuwa kundi la vijana ndio ambalo limekaa kwenye eneo hatarishi kutokana na yanapotokea machafuko mara nyingi wamekuwa wakiathirika na machafuko kutokana na wao kuwa mstari wa mbele pindi zinapotokea vita asilimia kubwa wamekuwa wakiathirika kwa kujua au kwa kutokujua.
“Tangu kuanza kwa mradi tayari tumepata vijana Zaidi ya 50 ambao wamefunzu kujua namna gani wanaweza kukutana na kundi la vijana wengine wakawaelimisha lakini pia vijana wetu wa Tanzania wamekuwa wakiawasiliana na vijana wa Rwanda,Burundi hali ambayo sasa tunaona kuwa ni fursa kwao kujuana na kujua ni namna gani wanaweza kuendelea kueneza Amani kwa nchi ambazo wanahishi tumegundua wakati mwingine hata mambo ya ukatili yanatokea kutokana na kukosekana kwa Amani”Jimmy Luhende Mratibu wa mradi wa Taifa wa nchi za maziwa makuu.