Home KITAIFA MRADI WA MAJI ULIOZINDULIWA NA CHADEMA WAUMIZA VICHWA

MRADI WA MAJI ULIOZINDULIWA NA CHADEMA WAUMIZA VICHWA

Njombe

CHADEMA kanda ya Nyasa kimemaliza ziara na mikutano kwa takribani siku 8 katika mkoa wa Njombe ambapo sambamba na mikutano jambo kubwa lililoacha maswali na kuumiza vichwa hususani kwa viongozi na Chama tawala ni zoezi la kuzindua mradi wa maji uliojengwa na wananchi wa kijiji cha Uliwa mjini Njombe.

Suala hilo limeonekana kuwashtua makada wa Chama cha Mapinduzi kwenye mitandao ya kijamii ambapo wameonekana wakihoji sababu za upinzani kuzindua mradi wa wananchi huku Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe Rose Mayemba akiendelea kutoa ufafanuzi kuwa hakuna kosa lililofanywa na Chama hicho kwa kuwa mradi ulianza kutokana na jitihada za wanachama wao baada ya kuona wakiteseka kwa kukosa maji.

Hata hivyo ikiwa imepita siku moja baada ya mradi huo unaotajwa kughalimu zaidi ya Milioni 20 na kuhudumia wananchi 150 wa vitongoji vya Canada na Itowa kuzinduliwa na mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Nyasa Peter Msigwa, baadhi ya wataalamu wamefika kijijini hapo ili kuzungumza na wananchi kutokana na mgogoro uliopo baina ya wafuasi wa CHADEMA,CCM pamoja na wale wasiokuwa na vyama kwa kuwa wote walishiriki kutoa michango yao.

Mbele ya uongozi wa Wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Njombe na viongozi ngazi ya kijiji na Kata ya Iwungilo waliofika kusikiliza malalamiko hayo baadhi ya wakazi akiwemo Valelia Manga,Emelda Mtewele na Salvius Mwalongo ambaye ni mwenyekiti wa kijiji cha Uliwa ambaye naye alichangia takribani shilingi laki mbili kwenye ujenzi wa mradi huo wanasema hawakukubaliana nani atauzindua hivyo walishangaa kuona CHADEMA wakizindua bila makubaliano ya pande zote.

Wananchi wengine akiwemo Sigfrid Msigwa,Longnus Mlowe na Casmiry Mgina mwenyekiti wa kamati ya ukusanyaji michango ya ujenzi wa mradi huo wamesema hawaoni sababu ya malumbano kwa kuwa wametaabika kwa kukosa maji hivyo viongozi wa serikali ngazi ya kijiji wanapaswa kuketi katika meza ya pamoja kuliweka sawa jambo hilo kwani hata Viongozi wa Chadema waliozindua mradi huo walitoa michango yao.

Germanus Ndumbaro Afisa mtendaji wa kata ya Iwungilo amesema hakuwa na taarifa ya uzinduzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho zaidi ya kupokea barua ya uwepo wa mkutano wa CHADEMA

Kwa upande wake Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Njombe Bakari Kitogota amesema kwa kuwa wananchi wamefikisha maji katika vitongoji viwili vya Itowa na Canada wao watafanya mpango wa kupeleka maji hayo katika vitongoji viwili vilivyosalia ambavyo vyote vinategemea chanzo kimoja na kwamba kama wakala watakwenda kupima maji hayo.

“Ili maji yawafikie lazima yapimwe yajulikane Uwingi na ubora,tulitakiwa tushirikiane na swala la uzinduzi wa mradi huwa unakuja kuzinduliwa na watu wa serikali”Alisema Kitogota

Previous articleDC ILEJE ATIMIZA AGIZO LA RAIS SAMIA
Next articleMMOMONYOKO WA MAADILI WAWALIZA WAHITIMU-KIDATO CHA SITA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here