Ikiwa Serikali pamoja na wadau wa Sekta binafsi wakiendelea kuboresha Sekta ya Afya Nchini ambayo utajwa kuzungukwa na changamoto mbalimbali, baadhi ya wananchi katika Kata ya Mkonze mkoani Dodoma wamefurahishwa na mradi wa Afya Shirikishi ambapo wamedai kuwa umewawezesha kufahamu wajibu wao katika ushiriki wa maswala ya afya pamoja na kuchochea uwazi na uwajibikaji katika kituo chao cha afya.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa elimu iliyotokewa katika mradi wa Afya shirikishi unaotekelezwa na Asasi ya kiraia ya Wajibika, Shadrak Lucas ambaye Mwenyekiti wa Kamati ya Afya Kata ya Mkonze, amesema kuwa elimu hiyo imepelekea wananchi kushiriki katika masuala ya afya ikiwemo kituo cha afya kwenye Kata hiyo kuanza kuweka baadhi ya mambo wazi ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji.
” Ndugu zetu Wajibika wametusaidia sehemu kubwa kabla hatujapata elimu waliotupatia tulikuwa hatujui vitu vingi lakini baada ya kupata semina na kufundishwa sisi kama wanajamii tunatakiwa tujuwe na kweli tumeona umuhimu, siku za nyuma ulikuwa ukienda kwenye kituo cha afya unakuta uwazi wa mapato na matumizi haupo lakini kwa sasa tuliporudi tumekuta wameweka lakini siku za nyuma walikuwa hawaweki” amesema
Upande wa mwakilishi wa wanufaika wa mafunzo hayo ambao yanatolewa na Wajibika, Christina Malogo, Mjumbe wa Kamati ya Afya Kata Mkonze amesema elimu wanayoipata imewaondolea hofu na kuchochea ushirikiano baina yao na wahudumu wa afya.
“Kwakweli tunashukuru Wajibika maana kipindi cha nyuma tulikuwa tunahisi tunanyanyaswa hatuwezi kuuliza chochote kwenye kituo cha afya, lakini sasa baada ya mafunzo hofu imeisha, kwanza tumkuwa marafiki na wale wahudumu wakina Mama wengi wanafurahi ilikuwa hata ukiona jambo ambalo sio rafiki huwezi kuuliza ” amesema Mjumbe huyo
Aidha kwa upande wa watekelezaji wa mradi huo, John Mwilongo ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Afya Shirikishi, kutoka Shirika la Wajibika amebainisha dhamira ya mradi huo akisema.
“Mradi huu lengo la kuimarisha mifumo, utoaji na upokeaji huduma za afya kupitia ushirikishaji wa watoa huduma na wapokea huduma na kwasasa mradi huo unatekelezwa kwenye Kata nne mkoani Dodoma ambazo ni Kata za Mkonze, Matumbulu, Ihumwa na Changombe kwa nyakati tofauti ikiwa tayari tumeanza na Mkonze”
John ameongeza kuwa “Tuliona kwanini kunakuwa na malalamiko ya wananchi kwamba nimeenda hospitali nimekuta huduma azilizishi, tukaona tuje na mradi huu ambao utajumuisha watoa huduma na wapokea huduma, hao wananchi wapate fursa ya kujifunza kwa karibu utoaji wa huduma kwenye vituo vyao ili wakienda pale wapunguze manunguniko ambayo yanaweza kuepukwa, lakini pia washiriki katika maendeleo ya kufanya maendeleo vituo vyao, kwa sababu watashiriki katika kupanga mipango ya kituo lakini pia watashiriki katika kutekeleza baadhi ya mambo pia watakuwa mabingwa (champion) katika kuelimisha wengine”
Wajibika ni taasisi ya kiraia inayofanya kazi kuimiza mifumo ya uwajibikaji katika sekta ya afya, Elimu na Kilimo, ambapo kwa sasa inatekeleza mradi mkoani Dodoma katika kitengo cha afya.