Home KITAIFA MPANJU AWASIHI VIONGOZI WA DINI KUIMARISHA MAFUNZO YA NDOA ILI KUIMARISHA MAADILI

MPANJU AWASIHI VIONGOZI WA DINI KUIMARISHA MAFUNZO YA NDOA ILI KUIMARISHA MAADILI

Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini wametakiwa kuimarisha mafunzo ya maadili kwa wanandoa kutokana na vitendo vingi vya ukatili na unyanyasaji kufanyika katika ngazi ya familia na kusababisha mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa jamii.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju alipokuwa akifungua warsha ya viongozi wa dini wa Mikoa mitano ya Kigoma, Rukwa, Katavi, Singida na Dodoma iliyofanyika Mkoani Kigoma Agosti 7, 2023.

Mpanju amesema uwepo wa migogoro ndani ya ndoa pamoja na wazazi wengi kutokutekeleza kwa ufasaha majukumu yao ya kimalezi kwa watoto wao, kumeendelea kusababisha kuibuka kwa wimbi kubwa la tabia na mienendo isiyoridhisha miongoni mwa wanajamii.

‘’Katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara tumeamua kuandaa mwongozo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini ili kutoa dira kwa wazazi na jamii kwa ujumla itakayowapa mwelekeo ili kupata namna bora ya kutoa malezi kwa watoto’’ amesisitiza Mpanju.

Aidha Mpanju amesisitiza uwepo wa umakini katika matumizi ya teknolojia na utandawazi ikiwemo kudhibiti mafunzo na uigizwaji wa tabia zinazoenda kinyume na mafundisho ya kiimani pamoja na Mila na Desturi za kitanzania.

Naye Shekhe wa Mkoa wa Dodoma Mustapha Rajabu amesema jamii inapaswa kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yatakayowaimarisha kimwili na kiroho na kuwafanya waishi maisha yenye uadilifu.

‘’Malezi kwa watoto wetu yaendane na upendo, upatikanaji wa huduma ya elimu dini na ile ya kidunia pamoja na uadilidhwaji mkubwa kuhusu namna bora ya kuishi’’ amesisitiza Shekhe Rajabu.

kwa upande wake Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma Joseph Mlola ameishukuru Wizara kwa hatua inazoendelea kuchukua kwa lengo la kurejesha misingi ya maadili katika Jamii.

Aidha Mlola amewasisitiza wajumbe wa kikao hicho navViongozi wenzake kufuatilia kwa ukaribu mada mbalimbali zitakazotolewa kisha kutoka na mapendekezo yatakayoleta mabadiliko yenye tija kwa taifa katika kulinda maadili.

Previous articleKAMARI JANGA HATARI VYUONI.. NDOTO ZA WANAFUNZI WENGI KUISHIA NJIANI KWA KUTUMIA ADA KWENYE KAMARI_ MAGAZETINI LEO JUMANNE TAREHE 8/08/2023
Next articleJAFO AYATAKA MABONDE YOTE NCHINI KUENDELEA KUHAMASISHA UPANDAJI WA MITI 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here