Mtu mmoja amefariki na wengine sita kujeruhiwa katika ajali iliyotokea usiku wa kuamkia Septemba 4 eneo la mataa ya Tumbaku Manispaa ya Morogoro barabara kuu ya Morogoro – Iringa ikihusisha lori la mizigo lenye namba T862 DNH lililokuwa linatokea Dar es salaam kwenda Iringa kugongana na basi la abiria lenye namba za usajili T 994 DCH lililokuwa linatokea kituo cha Mabasi Mafiga kwenda Msamvu.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema walisikia mlio mkubwa na waliposogelea eneo la tukio walikuta dereva wa lori amebanwa kwenye gari akivuja damu nyingi huku wasafiri waliokuwa kwenye basi la abiria wakipata majeraha.
Kaimu kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Morogoro Emmanuel Ochieng amesema,baada ya kufika katika eneo la tukio walifanya maokozi huku majeruhi wakiwapatia huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa hospitali ambapo amesema aliyefariki kwenye ajali hiyo ni dereva wa lori la mizigo na waliojeruhiwa ni abiria watano na dereva mmoja waliokuwepo kwenye basi la abiria,huku chanzo cha ajali kikitajwa ni uzembe wa dereva wa lori kuendesha kwa mwendokasi.