Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Door Of Hope Clemence Mwombeki amesema kuwa, ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto upo na unazidi kuongezeka na sababu kubwa ni wazazi kupunguza umakini kwenye swala zima la malezi.
Mwombeki amesema licha ya wanahabari,serikali na wadau mbalimbali kuweka jitahada kubwa ili kuhakikisha wanatokomeza ukatili wa kijinsia kwa jamii zetu ila bado vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto vinaongezeka kwa kasi siku hadi siku.
“Zaidi tumebaini changamoto kubwa ya ulawiti na ubakaji kwa watoto hapa nchini jambo ambalo linaongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi na limekuwa likiripotiwa kila eneo kila Mtaa, tatizo hili limekuwa likiendelea kukua zaidi kwasababu jamii yetu imekuwa ikilichukulia jambo hili kwa wepesi na kutochukua hatua lakini pia kuna changamoto kubwa sana ya wazazi kutoweka umakini kwenye malezi yao na kujikita zaidi kwenye shughuri za utafutaji.”
“Tunatatizo kubwa sana la mmong’onyoko wa maadili wazazi,watoto,viongozi na walimu wote wana mmong’onyoko wa maadili na tunapo zungumza watoto wa siku hizi pia tuangalie wazazi wa siku hizi wazazi hao wanaoishi kwenye mazingira na maisha ambayo hayana staha na usalama kwa watoto wetu.”Mwombeki amesema
Pia amewataka wazazi na jamii kwa ujumla kutoa taarifa kwa vyombo husika ili kutokomeza ukatili na kuacha kufumbia macho vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watoto kwani kumekuwa na baadhi ya wazazi/walezi kutotoa ushirikiano kesi inapofika mahakamani kwa lengo la kumficha muhusika.
Aidha Mwombeki amekiri kuongezeka kwa changamoto ya afya ya akili hivyo ameiomba Serikali kushirikiana na wataalamu wa saikolojia ili kuona namna ya kushughulikia jambo hili hususani katika ngazi za familia.