Na Theophilida Felician Kagera.
Kiongozi wa chama cha ACT WAZALENDO Mhe Zitto Zuberi Kabwe amesema kuwa hali ya kiwango cha umaskini wa Mkoa Kagera bado kiko juu mno.
Zitto ameyanena hayo wakati akiwahutubia wakazi wa mji wa Bukoba katika viwanja vya Uhuru Mayunga vilivyopo Manispaa ya Bukoba.
“Juzi wakati najiandaa na safari yangu yakuja huku Kagera nilikuwa nasoma taarifa ya ofisi ya takwimu ya taifa kuhusu walivyoipanga mikoa kulingana na pato la mtu mmoja mmoja nikakuta Mkoa wa Kagera ndiyo unashika mkia kwa pato la mtu mmoja mmoja, ni kwamba Mkoa wenu ndio maskini zaidi nchini” Zitto Kabwe akiwaeleza wananchi.
Amefafanua kuwa mnamo mwaka wa (1994) katika mikoa 21 ya Tanzania Bara Kagera ulikuwa Mkoa wa 12 kwa kipato( 2005) ukawa wa 19 mwaka (2022) umekuwa wa 26 kati ya mikoa 26.
“Mkoa wenu ni wa mwisho kwa kipato cha mtu mmoja mmoja, iweje mkoa wenu uwe maskini? ukiangalia Ardhi iliyopandwa mikahawa kwa wingi Tanzania nzima katika mikoa yote ni ni ardhi ya mkoa wa Kagera mnakuwaje maskini? Ukiangalia mkoa wenu ndio unaopakana na nchi nyingi zaidi za jumuiya ya Afrika mashariki mnapakana na Uganda, Burundi, Rwanda na Kenya kwa upande wa ziwa Victoria kwa maana hiyo ni kwamba huu Mkoa ungepaswa kuwa kituo cha biashara cha eneo la Afrika Mashariki kwanini Kagera iendelee kuwa maskini? nusu nusu ya wakazi wa Kagera mko chini ya mstali wa umaskini” Zitto Kabwe akiwaeleza bayana wananchi.
Aidha amesema kuwa chanzo cha umaskini wa mkoa huo moja wapo ni kudolola kwa shughuli za kiuchumi ambapo hakusita kukitaja chama cha (CCM) kuwa hakiwezi kukwepa lawama ya kudidimiza maendeleo ya wana Kagera hivyo amewasihi wananchi kutafuta mbinu mbadala ya kubadilisha mfumo wa uongozi utakaosaidia kuiondoa aibu hiyo ya umaskini hasahasa kuwachagua viongozi kupitia vyama pinzani tofauti na (CCM)
Kiongozi huyo pia amzungumzia juu ya jitihada zinazofanyika katika kuisaka katiba mpya itakayowezesha kuyalekebisha mambo yote ambayo hayako sawa hususani katika masuala ya uchaguzi huku akisisitiza kuwa sheria mpya ya uchaguzi iandikwe ili kuipa Uhuru tume ya uchaguzi ili iweze kusimamia kwa Uhuru uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu wa (2025.)
Hata hivyo amegusia changamoto ya uhaba wa upatikanaji wa vitamburisho vya taifa NIDA ilivyokuwa kubwa kwa wananchi wa Mkoa Kagera, ametoa wito kwa mamlaka husika kuhakikisha wanawapatia vitamburisho haraka iwezekanavyo kwani ni haki yao.
Juma Duni Haji Mwenyekiti wa chama hicho amewaeleza wananchi kwamba chama hicho kimejizatiti kufanya makubwa yakuwaeletea mageuzi makubwa ya kimaendeleo watanzania wote bila yakuwepo ubaguzi kama ilivyo kauli mbiu ya chama inayosema “TAIFA LA WOTE KWA MASLAHI YA WOTE”
Mwenezi wa chama ngazi ya Taifa Bi Janet Joel Rithe yeye amebainisha kuwa ACT ni chama kinachojipambanua zaidi kwa sasa katika kuwafikia wananchi na kuyahidi mambo mbalimbali yenye maslahi mapana kwa wananchi na nchi kwa ujumla hivyo amewaomba wananchi kukiamini na kukiunga mkono kwa nguvu zote hatimaye kiweze kushika dola katika chaguzi zijazo za serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu wa (2025)