Home KITAIFA MKATABA WA UJENZI WA BARABARA YA SENGEREMA-NYEHUNGE KM 54.4 WASAINIWA

MKATABA WA UJENZI WA BARABARA YA SENGEREMA-NYEHUNGE KM 54.4 WASAINIWA

Mgeni rasmi katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 kwa kiwango cha lami ambaye ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ,Mhandisi Godfrey Kasekenya akiongea wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Mnadani wilayani Sengerema mkoani Mwanza Aprili 23, 2023

Na Mwandishi wetu Sengerema, Mwanza

Serikali imesaini mkataba ujenzi wa barabara ya Sengerema hadi Nyehunge kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 54.4 ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi kama vile usafirishaji wa mazao ya misitu, mazao ya chakula, mazao ya uvuvi pamoja na mazao ya biashara na shughuli za kijamii kwa ujumla.

Mkataba uliosainiwa ni baina ya Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa niaba ya Serikali na mkandarasi AVM-Dilingham Construction International Inc aliyeshinda zabuni ambaye atajenga barabara hiyo kwa kipindi cha miezi 28 ambapo mradi mzima unagharimu kiasi cha shilingi 73,047,903,363.67.

Akiongea katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa mradi huo, iliyofanyika Aprili 23, 2023 katika viwanja vya Mnadani wilayani Sengerema mkoani Mwanza, mgeni rasmi katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amemtaka mkandarasi huyo kukamilisha ujenzi huo kwa viwango na wakati uliopangwa pamoja na kuzingatia thamani ya fedha ya mradi (Value for Money) wakati wa ujenzi.

Vilevile Mhandisi Kasekenya amiagiza TANROADS kusimamia mradi huo kwa udhibiti mkubwa ili barabara iweze kutumika kwa muda uliopangwa.

Mhandisi Kasekenya ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ni mkakati wa serikali kuboresha miundombinu huku fedha za utekelezaji wa mradi huo zikitoka serikalini kwa asilimia mia moja.

“Ujenzi wa barabara hii (Sengerema-Nyehunge kilometa 54.4 kwa kiwango cha lami) utafanyika kwa kutumia fedha za ndani kwa asilimia 100 na ni juhudi na mikakati ya Serikali katika kuboresha miundombinu yake” alisema Mhandisi Kasekenya na kuongeza

“Madhumuni ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami ni kuwaondolea wananchi kero ya usafiri wa barabarani na kuboresha mtandao wa barabara na madaraja ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji”

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akiongea katika hafla hiyo amesema, ujenzi wa barabara hiyo ni mradi wa kimkakati kwa Wana Mwanza hivyo kama uongozi wa mkoa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama watahakikisha wanaufatilia kwa karibu.

“Mradi wa Sengerema-Nyehunge ni mradi wa kimkakati kwa wana Mwanza, na kila mradi unaotekelezwa unakuwa na athari kwa mkoa mwingine katika nyanja mbalimbali” alisema Malima na kuongeza

“Ni kazi yetu kusimamia kuhakikisha kwamba mradi unakamilika kwa wakati”

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akitoa salamu za mkoa huo wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa Ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 kwa kiwango cha lami iliyofanyika katika viwanja vya Mnadani wilayani Sengerema mkoani Mwanza Aprili 23, 2023

 

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amesema, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Sengerema-Nyehunge ulifanywa na kampuni ya Inter Consult Ltd ya Tanzania kuanzia mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2020 kwa gharama ya shilingi 779,274,725.80

Kufuatia hilo, Mhandisi Mativila ametoa wito kwa mkandarasi kutekeleza mradi huo kwa weledi wa hali ya juu.

“Natoa wito kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huu kampuni ya AVM-Dilingham

Construction International Inc. kufanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu ili kazi zote zikamilike ndani ya muda uliopangwa na kwa viwango na gharama zilizokubalika” alisisitiza Mhandisi Mativila

Mtendaji Mkuu wa TANROADS ,Mhandisi Rogatus Mativila akitoa taarifa fupi kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 kwa kiwango cha lami katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Mnadani wilayani Sengerema mkoani Mwanza Aprili 23, 2023
Mtendaji Mkuu wa TANROADS ,Mhandisi Rogatus Mativila (kushoto) akiwa na mkurugenzi wa kampuni ya AVM-Dilingham
Construction International Inc. ya nchini Uturuki, wakionesha hati za mikataba waliotiliana saini leo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 kwa kiwango cha lami.
Hafla ya utiaji saini wa mradi huo imefanyika katika viwanja vya Mnadani wilayani Sengerema mkoani Mwanza Aprili 23 ,2023

Wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 kwa kiwango cha lami.
Hafla ya utiaji saini imefanyika katika viwanja vya Mnadani wilayani Sengerema mkoani Mwanza Aprili 23 ,2023

Kwa upande wao wabunge wa majimbo ya Sengerema na Buchosa , Hamis6 Tabasamu na Eric Shigongo ambao ni wanufaika wa barabara hiyo, wameishukuru serikali kupitia mradi huu uliosainiwa na kusema kilio cha muda mrefu kuhusu changamoto ya barabara hiyo kimeisha na hivyo wananchi wao wamejipanga tayari kutumia fursa ya ujenzi wa barabara hiyo .

Mbunge wa jimbo la Sengerema, Hamis Tabasamu akiongea wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa Ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 kwa kiwango cha lami
Mbunge wa jimbo la Buchosa, Eric Shigongo akiongea wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa Ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 kwa kiwango cha lami iliyofanyika katika viwanja vya Mnadani wilayani Sengerema mkoani Mwanza Aprili 23, 2023

Nao wananchi Aneth Sixstus, Peter Poteza na Maimuna Ramadhani wameishukuru serikali kwa kuwajengea barabara hiyo na hivyo itawarahisishia usafirishaji wa mazao yao na pia kuondokana na adha ya ugumu wa usafiri wakati wa kipindi cha masika.

Wananchi mbalimbali wakiwa wamejitokeza katika viwanja vya Mnadani wilayani Sengerema mkoani Mwanza kushuhudia tukio la utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 kwa kiwango cha lami Aprili 23, 2023

Barabara ya Sengerema-Nyehunge yenye urefu wa kilometa 54.4, ni moja ya barabara muhimu katika mtandao wa barabara muhimu za Mkoa wa Mwanza na inaiunganisha Mkoa wa Mwanza na mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita.

Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ulifanywa na kampuni ya Inter Consult Ltd ya Tanzania kuanzia mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2020.

Mwonekano wa barabara ya Sengerema-Nyehunge KM 54.4 ilivyo hivi sasa, ambapo inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami kufuatia mkataba wa mradi wa ujenzi huo kusainiwa Aprili 23, 2023 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 28
Previous articleRAIS DKT. SAMIA: TUMEPITIA WAKATI MGUMU KUFIKIA UMOJA NA MSHIKAMANO _ MAGAZETINI LEO JUMAPILI APRILI 23/2023
Next article“PELEKENI WATOTO KUPATA CHANJO KUWAKINGA NA MAGONJWA_ PROF. NAGU

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here