NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imemhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela Bahati Kafwile (25) fundi ujenzi na mkazi wa Iwambi jijini Mbeya baada ya kupatikana na kosa la Unyang’anyi kwa kutumia silaha huku mwenzake akiachiwa huru.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Sangiwa Mtengeti, wakati akisoma shauri la jinai namba 99/2022 lililokuwa likiwakabili Bahati Kafwile (Bahati Ngole) na Yusuph Abraham kwa mashtaka mawili ya Unyang’anyi wa kutumia silaha na kupatikana na mali idhaniwayo kuwa ya wizi.
Hakimu Mtengeti amesema Mahakama yake imeridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa Jamhuri kuwa mshtakiwa alitekeleza unyang’anyi huo kwa kutumia silaha baada ya kutumia nondo kumtishia mlalamikaji aitwaye Tiberio Kitindi kisha kumpora mali vitu mbalimbali ikiwemo simu na begi.
Hakimu huyo amesema ushahidi huo hasa wa mlalamikaji na maofisa wa polisi unadhihirisha mtu huyo kutekeleza uahalifu huo kwa njia ovu badala ya kujikita kwenye ufanyaji kazi ili kujipatia kipato halali licha ya kwamba kwenye utetezi wake mshtakiwa Bahati alikana kutenda kosa hilo na akaiomba mahakama kumpunguzia adhabu.
Mwendesha mashtaka wa Serikali Michael Bajuta ameiomba mahakama kutoa adhabu kali ili kusaidia kukomesha matukio ya uhalifu.
Baada ya kuridhika na ushahidi huo wa Jamhuri bila kuacha shaka yoyote Hakimu Sangiwa Mtengeti ameelekeza mwananchi Bahati Kafwile kwenda jela miaka 30 ili iwe fundisho kwake na jamii kwa ujumla kutokana na vitendo vya wizi kuzidi kushamiri katika jamii.
Kwa mujibu wa Hati ya Mashtaka Mshtakiwa Bahati alitekeleza uhalifu huo Mei 20, 2022 katika eneo la Lumbila Iwambi jijini Mbeya baada ya kuiba simu moja aina ya Tecno, koti moja, begi moja na fedha Sh.2500 mali ya Tiberio Kitindi akitumia silaha aina ya nondo kumtishia mwananchi huyo ili kujipatia vitu hivyo kosa ambalo ni kinyume na kifungu namba 287 A cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Mshtakiwa wa pili Yusuph Abrahamu mkazi wa Mapelele Mbalizi alikuwa akishtakiwa kwa tuhuma za kupatikana na mali za wizi ambayo ni simu aliyoinunua kwa mshtakiwa namba moja mali ya mlakamikaji kinyume na kifungu namba 312 (1) (b) ambapo hata hivyo ameachiwa huru.