Home KITAIFA MGODI WA MINJINGU WAPAISHA UKUSANYAJI WA MADUHULI MANYARA

MGODI WA MINJINGU WAPAISHA UKUSANYAJI WA MADUHULI MANYARA

 

 

Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Manyara, Mhandisi Ernest Sanka amesema kuwa mgodi wa Minjingu unaojihusisha na uchimbaji wa malighafi kwa ajili ya kuzalisha mbolea, pamoja na uzalishaji wa mbolea uliopo mkoani Manyara umechangia kwa asilimia 45 ya makusanyo ya maduhuli ya Tume ya Madini katika kipindi cha miaka miwili na kuitaka migodi mingine kuwekeza katika mkoa huo ili kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuunufaisha mkoa na kuzalisha ajira zaidi.

 

Mhandisi Sanka ameyasema hayo leo kwenye ziara katika mgodi huo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii katika Kanda ya Kaskazini.

Amesema kuwa, sambamba na mchango wake mkubwa kwenye ukusanyaji wa maduhuli, mgodi umefungua fursa nyingine za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuzalisha bidhaa bora ya mbolea ambayo hutumika kwa ajili ya kilimo nchini na nyingine kusafirishwa nchi za jirani za Uganda, Kenya na Burundi sambamba na kuajiri wafanyakazi wa kitanzania kutoka katika mkoa wa Manyara na mikoa mingine.

 

Katika hatua nyingine, Mhandisi Sanka amewataka wawekezaji wengi zaidi kujitokeza na kuwekeza katika shughuli za uchimbaji wa madini katika mkoa wa Manyara kutokana na mkoa huo kubarikiwa madini ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya metali, viwandani, ujenzi na vito.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Minjingu, Mahesh Parik akielezea namna mgodi ulivyojipanga katika kuwawezesha watanzania kiteknolojia amesema kuwa mgodi umekuwa na programu maalum ya uhawilishaji wa teknolojia ( _technology transfer)_ ya kuwapa watanzania teknolojia ya kisasa ya uendeshaji wa mgodi ili baadaye waweze kuwa waendeshaji wakuu wa mgodi.

Previous articleSPIKA WA BUNGE AOMBA JIMBO LAKE LA MBEYA MJINI LIGAWANYWE
Next articleCHARLES HILLARY: UZOEFU KWENYE UANDISHI WA HABARI KUSIKUFANYE UACHE KUJIFUNZA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here