Home KITAIFA MFUKO WA DUNIA KUENDELEA KUFADHILI AFUA ZA KUPAMBANA NA UKIMWI, MALARIA NA...

MFUKO WA DUNIA KUENDELEA KUFADHILI AFUA ZA KUPAMBANA NA UKIMWI, MALARIA NA KIFUA KIKUU NCHINI

NA. MWANDISHI WETU

Serikali imepongeza jitihada zinazofanywa na Mfuko wa Dunia katika kufadhili miradi inayotekelezwa kwenye afua za kupambana na UKIMWI, Malaria, Kifua Kikuu pamoja na uboreshaji wa mifumo ya utoaji wa huduma za afya nchini kwa lengo la kuendelea kuwa na huduma bora za afya.

Pongezi hizo zimetolewa hii leo Juni 9, 2023 na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Crispin Musiba alipotembela na kukagua utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Dunia katika mkoa wa Tabora ambapo walitembelea Hospitali ya Mkoa huu ya Kitete pamoja na kukagua utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa jengo la maabara katika Hospitali ya Mji Nzega.

Bw. Musiba amesema kuwa, ufadhili wa miradi hiyo umeendelea kuleta tija kwa jamii kwa kuzingatia kuwa huduma zinapatika kwa ubora na kuwa na vifaa vinavyosaidia masuala ya kitabibu.

“Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo mratibu wa shughuli hii, hivyo tumeweza kujionea maendeleo ya miradi yote hususan namna vifaa vilivyonunuliwa, upanuzi wa maabara katika viwango vizuri ambapo tunaamini mradi utaendela kulifaa Taifa pamoja na mkoa kuendelea kutatua changamoto chache zilizo ndani ya uwezo wa mkoa,”aslisema Musiba

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Kamati ya Kitaifa inayoratibu na kusimamia fedha kutoka Mfuko wa Dunia (Global Fund) TNCM Dkt. Rachel Makunde ameseama ziara imeongeza tija na umuhimu wa kujionea namna mradi unavyotekelezwa kwa kuzingatia malengo yanayokusudiwa.

“Utekelezaji wa afua zilizochini ya Mfuko wa Dunia, zimeendelea kuzaa matunda kwa kuangalia hii ya ujenzi wa emergency department, pamoja na chumba cha maabara katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora ya Kitete pamoja na hii ya Nzega, kazi inaenda vizuri na ujenzi wa maabara hapa Nzega inaridhisha,”

Aliongezea kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu na kusimamia kwa weledi maeneo yanayotekelezwa miradi hii ili kuendelea kutoa huduma bora za kiafya kwa wananchi wote.

Aidha alipongeza juhudi za mkoa kwa kutumia vyanzo vya mapato vya ndani katika ununuzi wa samani zilizohitajika katika Hospitali ya mkoa pamoja na chanagamoto kadhaa wanazokabiliana nazo.

“Global fund itaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali, ninapongeza namna mkoa unavyokabili na kuboresha maeneo yaliyo na changamoto, kwa hapa Nzega jengo la maabara linaendelea vizuri lipo hatua za mwisho na lenye viwango vizuri hivyo thamani ya fedha zilizotolewa zinasadifu,”alisema Dkt. Rachel

Akizungumzia ziara hiyo Dkt. Rachel amesema,imelenga kutembelea mikoa sita ikiwemo wa Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Singida na Dodoma ikiwa ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza miradi hiyo.

Previous articleDKT. TAX AKUTANA NA NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA WA ITALIA JIJINI ROMA
Next articleNAIBU CAG ZANZIBAR AAPISHWA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here