Home KITAIFA MENEJA TANROADS KIGOMA: KILOMETA 420 ZA BARABARA KWA KIWANGO CHA LAMI KUJENGWA...

MENEJA TANROADS KIGOMA: KILOMETA 420 ZA BARABARA KWA KIWANGO CHA LAMI KUJENGWA KWA MARA MOJA, HAIJAWAHI KUTOKEA

Meneja wa TANROADS Mkoa Kigoma, Mhandisi Nacris Choma akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Kigoma mbele ya waandishi wa habari Aprili 21, 2023

 

Na Mwandishi wetu, Kigoma

Historia katika upande wa uboreshaji wa miundombinu ya barabara imeandikwa katika Mkoa wa Kigoma kufuatia ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 420 kujengwa kwa mara moja katika mkoa huo ili kuunganisha mkoa huo na mikoa ya jirani pamoja na nchi jirani jambo ambalo halijawahi kutokea.

Hayo yamesemwa Aprili 21, 2023 na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Nacris Choma akiongea na waandishi wa habari ambapo amesema ujenzi wa barabara hizo unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 567.

Meneja wa TANROADS Mkoa Kigoma, Mhandisi Nacris Choma akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Kigoma mbele ya waandishi wa habari Aprili 21, 2023

Kufuatia hilo, Mhandisi Choma ameishukuru serikali ya awamu sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea miradi na fedha za utekelezaji wa miradi hiyo ambapo tija yake imeonekana.

“Tunaishukuru serikali kwa kutuletea miradi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika Mkoa wa Kigoma, Kigoma sasa inafunguka, na niwakaribishe wananchi mje kuwekeza katika Mkoa wa Kigoma” alisema Mhandisi Choma

Ameendelea kwa kusema kuwa, Serikali ya awamu ya sita imeutazama Mkoa wa Kigoma kwa jicho la kipekee na hivyo kuufanya mkoa huu kupaa katika nyanja mbalimbali ikiwemo ukuaji wa uchumi.

Mwonekano wa round about (kikuta shoto) katika eneo la Kabingo. Round about hiyo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Nduta hadi Kabingo (KM 62.5) kwa kiwango cha lami
Moja ya madaraja yaliyojengwa katika ujenzi wa barabara ya Mvugwe hadi Njia Panda wilayani Kibondo yenye urefu wa kilometa 59.35

Kazi mbalimbali za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwa zinaendelea mkoani Kigoma
Mwonekano wa baadhi za barabara zikiwa zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami mkoani Kigoma

Kando na miradi hiyo, kuna miradi 9 ya usanifu katika mkoa huo ikiwemo mradi wa uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Kigoma .

Kuhusu uboreshaji wa mradi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, Mhandisi Choma amesema

“Katika uboreshaji huu kutajengwa jengo jipya la abiria, sehemu ya kupaki ndege (apron), tutajenga barabara za kuelekea uwanja wa ndege, mnara wa kuongoza ndege, ujenzi wa ofisi ya zimamoto, kituo kidogo cha kupoza umeme na uzio. Na kwa upande wa njia za kuruka na kutua ndege tutaweka taa ili kuwezesha ndege kutua na nyakati za usiku na mkandarasi wa mradi huu yupo tayari eneo la Mradi (site)”

Hata hivyo, ametoa wito wa wananchi pamoja na watumiaji wa barabara kuwa walinzi wa miundombinu ya barabara na hii ni kufuatia matukio ya watu wasio waaminifu kuiba alama za barabarani, kuchimba barabara zilizokamilika pamoja na kupitisha mifugo.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Matengenezo TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe ameeleza kuwa, Mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Manyovu-Kasulu-Kibondo-Kabingo, ina urefu wa kilometa 260.6, ambapo mradi huo unaanza katika mpaka wa Tanzania na Burundi, mpakani ambapo kutakuwa na Kituo Cha Huduma Cha Pamoja Mpakani (OSBP) na vitajengwa vituo viwili kimoja upande wa Burundi na kingine upande wa Tanzania.

Mkuu wa Idara ya Matengenezo TANROADS Mkoa Kigoma, Mhandisi Ngoko Mirumbe akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Manyovu-Kasulu-Kibondo-Kabingo yenye urefu wa kilometa 260.6

Akieleza faida za ujenzi wa vituo hivyo viwili kimoja Tanzania na kingine upande wa nchi ya Burundi na uwepo wa Kituo cha Huduma Cha Pamoja Mpakani, Mhandisi Mirumbe amesema

“Ukiwa upande wa Burundi utafanya taratibu za safari na utapewa vibali na utaendelea moja kwa moja na safari bila kusimama upande wa Tanzania, na hivyo hivyo ukiwa Upande wa Tanzania utafanya taratibu za safari na hautasismamishwa tena upande wa Burundi na utendelea na safari, katika vituo hivyo kutakuwa na wafanyakazi wote wa Burundi na Tanzania”

Mhandisi Mirumbe ameongeza kuwa, kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao na bidhaa nyingine kwa muda mfupi na kuuungansha Mkoa wa Kigoma na mikoa jirani ikiwemo Mwanza

Wakiongea kwa nyakati tofauti wananchi kuhusu ujio na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Kigoma wameeleza faida mbalimbali wanazopata na huku kutoa shukrani pamoja na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi hiyo ambayo imewanufaisha.

Dereva katika stendi ndogo ya Mvugwe wilayani Kasulu, Bw. Nickson James, amesema baada ya maboresho ya barabara ya Mvugwe kwenda Kanyani kwa sasa anaweza kufanya safari mara nyingi huku akichukua muda mfupi kwenda na kurudi.

Wakiongea kwa nyakati tofauti Kessy Mabirika na Sadock Poteza, wameipongeza serikali kufuatia utekelezaji wa mradi wa Manyovu-Kasulu-Kibondo-Kabingo ambapo wamesema kukamilika kwa miradi hiyo kutashusha gharama za usafiri pamoja, kuokoa muda wakati wa usafiri pamoja na kuchochea ukuaji wa biashara hususan wa zao la ndizi na hivyo kuwaongezea kipato.

Mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Manyovu-Kasulu-Kibondo-Kabingo yenye urefu wa kilometa 260.6 unatarajiwa kukamilika Desemba 17, 2023 ambapo katika utekelezaji kumepatikana faida lukuki za kijamii kupitia miradi ya nyongeza (complimentary projects) ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, ukarabati wa hospitali, ujenzi wa shule na stendi katika halmashauri ya wilaya ya Buhigwe, wilaya ya Kasulu na wilaya ya Kibondo ambapo miradi hiyo kwa pamoja inagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 21.

Previous articleWATUHUMIWA NANE (8) WAKAMATWA KWA MAKOSA MBALIMBALI MKOANI TANGA
Next articleUFAFANUZI KUHUSU KINACHODAIWA MTOTO KUGEUKA JIWE WILAYANI MUSOMA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here