Na Joel Maduka,Kahama.
Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe. Iddi Kassim Iddi leo Oktoba 04, 2023 amesisitiza kuwa ataendelea kuinua sekta ya Michezo katika Jimbo la Msalala.
Mhe. Iddi ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya kufunga mashindano ya IDDI CUP kata ya Chela ambapo ametaja baadhi ya jitihada anazoendelea kuzifanya ikiwemo kufadhili mashindano ya mpira wa miguu huku pia akinuia kuongeza nguvu kwenye soka la wanawake ili nao wapate fursa ya kuburudika na pengine kupata ajira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kahama ndugu Thomas Myonga amempongeza Mhe. Iddi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuunganisha wananchi wa Jimbo la Msalala kupitia mashindano hayo aliyoyafadhili ambapo pia Ndugu Myonga amewataka wananchi wa kata hiyo kuendelea kumuunga mkono Mhe. Iddi ili aweze kutimiza malengo yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo la Msalala.
Mashindano hayo katika kata ya Chela yamefikia tamati leo ambapo ulishuhudiwa mchezo wa fainali uliozikutanisha timu za NEW VISION FC dhidi ya MEDICAL FC ambapo timu ya NEW VISION imefanikiwa kushinda mchezo huo kwa bao moja na hivyo kujitwalia zawadi ya ng’ombe mnyama pamoja na Tsh elfu themanini huku timu ya MEDICAL FC wakiambulia Tsh Laki moja na nusu kwa kumaliza washindi wa pili wa mashindano hayo.