Home KITAIFA MBUNGE SUBIRA MGALU ATOA ELIMU NA UFAFANUZI WA VIFUNGU MKATABA WA BANDARI,...

MBUNGE SUBIRA MGALU ATOA ELIMU NA UFAFANUZI WA VIFUNGU MKATABA WA BANDARI, AONYA UBAGUZI DHIDI YA RAIS SAMIA

 

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

Ikiwa ni siku moja tu imepita tangu Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) itoe maazimio yake hususan azimio la kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo kwenye makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari azimio hilo limeanza kutekelezwa.

Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu ameanza kutekeleza azimio hilo kwa kutoa elimu na ufafanuzi wa kifungu kwa kifungu kwa wananchi wa kijiji cha Talawanda kata ya Talawanda wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Julai 10, 2023 kijijini hapo

Akiongea katika mkutano huo, Mheshimiwa Mgalu amesema, kuna baadhi ya watu wanahoji juu ya ukomo wa muda wa mkataba na kwamba katika hatua ya sasa muda mahususi wa mkataba hauwezi kutajwa lakini utakapofika wakati wa kusaini mikataba ya utekelezaji ndio muda wa mkataba utatajwa

“Wapo wanaouliza mkataba wa bandari utaisha lini na kwanini hauna muda mahususi, jibu lake ni kwamba huwezi kutaja muda mahususi katika mkataba wa awali wa ushirikiano baina ya Nchi (IGA ) kwani kuna hatua inayofuata ya mkataba wa nchi mwenyeji (HGA ) na mikataba ya utekelezaji humo ndipo muda wa utekelezaji wa miradi utatajwa” alisema Mgalu

Vilevile Mgalu amewatoa hofu wananchi hao kwa kueleza kuwa, hadi hivi sasa bandari haijauzwa na wala hakuna mkataba wowote uliongiwa kwa ajili ya shughuli za bandari ambapo amebainisha kuwa, mkataba uliowasilishwa bungeni mwezi uliopita ni mkataba wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai wenye lengo la kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.

Mgalu ameendelea kwa kusema kuwa, mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai juu ya uendelezaji wa bandari ya Dar es Salaam umetoa fursa ya maboresho kinyume kabisa na wanaodai kwamba ukishasaini mkataba huo hakuna marekebisho wala maboresho yoyote yatakayofanyika.

“Mkataba huu ni makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai juu ya uendelezaji wa bandari ya Dar es Salaam umetoa fursa ya maboresho kukiwa na haja na kukubalika pande zote na hilo limeelezwa katika ibara ya 22 ya mkataba huo” alisisitiza Mgalu

Akiongelea kuhusu kuwepo kwa baadhi ya wanaotoa maoni yao kuhusu suala la bandari na kuelekea kwenye kutoa kauli za ubaguzi dhidi ya Rais na viongozi wengine wa serikali, mbunge Mgalu amesema

“Tunaunga mkono maoni yote yenye nia ya kuboresha jambo hili (la uwekezaji wa bandari) lakini maoni yenye nia ya kuleta ubaguzi wa dini, rangi, kabila hayo sisi wana Bagamoyo hatuyaungi mkono. Ukosoaji wa suala la bandari unapokelewa lakini si ukosoaji unaotweza utu na heshima ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kama mama na kielelezo cha Taifa letu na Viongozi waandamizi ndani ya Serikali yetu, hili halikubaliki”

Bila kumtaja jina, mbunge Mgalu ameeleza kuwa, yupo mwanasheria mzoefu tu anadanganya watu kwamba mwekezaji (DP World) hatatozwa kodi, wakati huo huo anatambua wazi kuwa ibara ya 18 ya mkataba iinaelezea kodi, ushuru na tozo zote zitatozwa kwa mujibu wa sheria za kodi zilizopo nhini.

Kifungu namba 14 cha mkataba kimeleezea masuala ya utaifishaji, pale inapotokea mazingira fulani fulani serikali ya Tanzania inaweza kutaifisha uwekezaji kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa. Mbona vifungu hivi vipi na hamvitaji

“Kifungu namba 5 (4) cha mkataba kimeeleza ndani ya miezi 12 tangu kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano kama mkataba wowote wa utekelezaji haujaanza, basi mkataba utakuwa umeexpire. CCM tuko vizuri na tunajitambua, hivyo tumepitisha kitu tunachokitambua mkataba huu kwa maslahi ya nchi yetu” alihitimisha Mgalu

Previous articleTAWA YAPONGEZWA KWA KUENDELEZA UTALII WA MALIKALE
Next articleWATAKWIMU NCHINI WAMETAKIWA KUWA NA UWEZO WA KUCHAMBUA NA KUTAFSIRI MATOKEO YA SENSA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here