Home KITAIFA MBUNGE NJEZA AENDELEA NA ZIARA, UBOVU WA BARABARA BADO SHIDA MBEYA VIJIJINI

MBUNGE NJEZA AENDELEA NA ZIARA, UBOVU WA BARABARA BADO SHIDA MBEYA VIJIJINI

 

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Katika kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira na watoto kujiingiza kwenye uhalifu wananchi wa kijiji cha Kimondo Kata ya Igoma wameanza ujenzi wa chuo cha Veta ili watoto wao wasioendelea na masomo ya juu wakasome masomo ya ufundi stadi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimondo amesema waliamua kuanza ujenzi chuo hicho ili kuwasaidia watoto wanaoshindwa kufaulu kidato cha nne na darasa la saba kujifunza mambo mbalimbali.

Diwani Kata ya Igoma Andrew Mwaipopo amewashukuru wananchi waliotoa eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha ufundi stadi katika kijiji cha kimondo na kuiomba Serikali kuendelea kutoa fedha ili kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo uboreshaji barabara ambazo bado ni tatizo ikiwemo ya Isyonje hadi Makete mkoani Njombe.

Akizungumza baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa jengo kubwa la kwanza, Mbunge Oran Njeza amewapongeza wananchi kwa kushikamana kwenye shughuli za maendeleo ambapo amesema katika ujenzi wa chuo hicho cha ufundi Serikali itawaunga mkono huku naye akiahidi kuchangia shilingi million moja.

Pia amesema Serikali ina dhamira ya kuwatatulia kero zinazowakabili ikiwemo kwenye afya, maji na barabara ikiwemo ya Isyonje Makete ambayo bajeti ilishatengwa na fedha zinaendelea kutafutwa.

Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho chenye ilani inayotekelezwa kinasema kinajivunia kuona miradi inaendelea kujengwa na kuwataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kwa kero chache ambazo bado zinawakabili kikiahidi kuendelea kuzishughulikia. Msafiri Mwashambwa ni mjumbe wa kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Mbeya vijijini kwa niaba ya chama anasema CCM kinaridhishwa na utekelezwaji miradi hiyo.

Mbunge wa Mbeya Vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza anaendelea na ziara kwa kukagua miradi mbalimbali ikiwemo afya, elimu na barabara na katika Kata mbalimbali ambapo Zahanati ya Igoma inaendelea kuboreshwa kuwa Kituo cha afya hapo baadaye kwa kuendelea kujenga majengo ya Wagonjwa wa nje, jengo la Baba, mama na mtoto, jengo la OPD na Nyumba ya kuhifadhia maiti (Mochwari) ambayo tayari imekamilika.

Mwisho..

Previous articleDC ILEJE ACHAFUKWA USIMAMIZI MBOVU MIRADI YA BOOST
Next articleSHULE YA MWALIMU NYERERE YAWAFUNDA VIONGOZI WANAWAKE WA TAASISI NCHINI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here