MBUNGE MBEYA VIJIJINI AENDELEA NA ZIARA
NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amekutana na kufanya kikao na wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi (Kata za Nsalala na Utengule Usongwe) wilayani Mbeya akiwahimiza kuendelea kushikamana kuelekea chaguzi zijazo.
Pia Njeza amewahimiza kuwa chachu ya kueleza mambo mengi yanayofanywa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri kuu kutoka kata za Nsalala na Utengule Usongwe Mbalizi ambapo pia amewaasa kuendelea kujiandaa na mapokezi ya Rais Samia Suluhu Hassan anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Maonyesho ya sikukuu za wakulima Nanenane 2023 yanayoendelea kitaifa mkoani Mbeya.
Mbunge huyo wa Mbeya vijijini ambaye pia ni Mwenyekiti wa wabunge wa mkoa wa Mbeya amewaasa Madiwani katika Jimbo lake kuwa na utaratibu wa kuwasomea wananchi utekelezwaji wa Ilani yao (CCM) ili wajue Serikali inavyowatumikia katika kada mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu, Maji, Barabara na Umeme.
Kuhusu Uchaguzi ujao.
Mbunge wa Jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manase Njeza amewataka Viongozi wa Matawi na Kata wa CCM Wilaya ya Mbeya vijijini (kichama) kujiandaa na Uchaguzi wa Serikali za vijiji na vitongoji wa 2024 kwa kuhakikisha wanaandaa wagombea wenye uwezo wa kujitoa kupambana na kuhakikisha inawatumikia wananchi ili kufikia maendeleo endelevu.
Njeza amewatahadharisha Viongozi hao hasa ngazi za Matawi na Kata kuacha makundi yasiyo na msingi, maneno na tabia nyingine zisizo na tija katika kujenga umoja na mshkamano thabiti ulioasisiwa na Chama hicho kusimamia ukweli na uwajibikaji katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli ili kuibuka kidedea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa (2024) na baadaye uchaguzi mkuu (2025).
Kaimu katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Mbeya vijijini William Simwali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM wilayani humo amesema Chama hicho kinaridhishwa na utekelezwaji wa miradi katika jimbo la Mbeya vijijini inayoendelea kupeperushwa na madiwani, Mbunge Oran Njeza na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anayosema azma ya CCM ni kuendelea kuisimamia Serikali kuwatumikia wananchi wake.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mbeya Mwal. Anthony Mwaselela, amewapongeza wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Kata za Utengule Usongwe na Nsalala kwa kuendelea kushirikiana katika kuisimamia Serikali na kuhakikisha viongozi wao wanawajulisha wananchi utekelezwaji wa Ilani ya CCM katika maeneo yao (Vijiji na Kata).