NA JOSEA SINKALA, MOMBA-SONGWE
Mbunge wa Jimbo la Momba Mkoani Songwe Mhe. Condester Michael Sichalwe (Mundi) amewatembelea wananchi wa Kijiji cha Iyendwe Kata ya Kapele na kuwaasa kuuza mazao ya Chakula kwa utaratibu mzuri kwani njaa bado ipo.
Mhe. Condester Sichalwe amesema hayo katika Kijiji cha Iyendwe baada ya kuhudhuria msiba wa baba yake mkubwa Ndugu Sichalwe (76) uliotokea Julai 21, 2023 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Vwawa mkoani humo.
Condester amewasisitiza wananchi wa Iyendwe kujitokeza kwa wingi kuandikisha majina yao ioi kupata mbolea ya ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia maafisa kilimo wanaopita kuchukua idadi ya wakulima ili wapate mbolea ya ruzuku kwa bei elekezi ya Serikali.
Mbunge huyo amesema kuwa Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Skimu ya umwagiliaji hivyo amewaomba wananchi kuhudhuria vikao vya kupewa Elimu ya umwagiliaji inayotolewa na tume ya umwagiliaji kwenye Vijiji na Vitongoji vyao.
Aidha, amekemea vikali vitendo vya kuchoma moto misitu na mashamba yenye mazao kwani kumekuwa na kesi nyingi kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji juu ya kuchomeana mashamba kwakuwa musimu wa mavuno bado haujaisha hivyo wananchi wawe makini wanapowasha moto wa kupikia mashambani.
Mwisho, Mbunge Condester Sichalwe amewashukuru wana Kijiji cha Iyendwe kwa faraja katika msiba wa baba yake mkubwa na kuwakumbusha kupima afya mara kwa mara ili magonjwa yanayoepukika yapatiwe tiba na kuepusha vifo visivyo vya lazima katika Kijiji cha Iyendwe.