NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Waleta maombi ya shauri namba 05/2023 la Kupinga mkataba wa Bandari Wakili Alfonce Lusako na wenzake watatu wameiomba Mahakama kuu Kanda ya Mbeya kutengua mkataba wa Bandari ambao Serikali ya Tanzania imeingia na Kampuni ya DPW ya Dubai kwa madai kuwa mkataba huo ni batili, hauna sifa wala maslahi kwa Tanzania.
Waleta maombi wameeeleza hayo kupitia mawakili wao ambapo wakili mmojawapo Mpale Mpoki amesema maombi yao yana sababu mbalimbali za madhaifu ya mkataba huo ambao haukuwa shirikishi kwa wananchi na kupitishwa bungeni ni kukinzana na ibara 1, 8, 18 (d), 21[2] 27 ya katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Upande wa waleta maombi kupitia wakili Mpoki unasema kifungu namba 6 (2) 7 [2], 23 [4] kinaathiri usalama wa nchi jambo ambalo halikubaliki kwa Taifa.
Kwa upande wake Wakili Boniface Mwabukusi wa upande wa walalamikaji pia anaiomba mahakama kutengua maamuzi ya kusainiwa mkataba wa Bandari kwa maelezo kuwa unakinzana na vifungu mbalimbali vya katiba ya nchi ikiwemo ibara namba 4 (2) za usimamizi na ulinzi wa raslimali za nchi na kwamba mkataba unaonyesha kuwa Tanzania itakuwa ikiwajibika kwa Dubai katika uwekezaji huo hivyo anasema pamoja na matatizo mengine lakini mkataba huo haujakidhi vigezo vya kisheria hivyo ni batili.
Wakili Livino Ngalimitumba anasema mkataba huo ni hatari kwa nchi na una ukiukwaji wa moja kwa moja na inaondoa ukuu wa nchi hivyo ibara husika ya mkataba inavunja katiba akisema pia Tanzania haitakuwa na mamlaka ya kuvunja mkataba huo isipokuwa kwa sababu za kiusalama napo kwa masharti huku Tanzania ikionekana kuzuiwa kuingilia eneo ambalo DP World itawekeza hata kama ni sababu za kiusalama mambo yanayoondoa ukuu wa Tanzania.
“Waheshimiwa majaji kutoa Exclusive rights kwa DP World ni kuikosesha nchi yetu kujilinda na kulinda raslimali za nchi maana hakuna reservation rights. Ni maoni yetu (Walalamikaji) kwamba Mahakama ione kwamba kifungu namba 5 (1) kinakiuka ibara ya 28 ya Katiba ya Tanzania na ione hiyo ni sababu ya kubatilisha mkataba wa IGA”, Wakili Livino Ngalimitumba.
Wakili Phillip Mwakilima wa walalamikaji anakosoa sheria ya manunuzi namba 64 haikuzingatiwa kwani hakuna mahali panapoonyesha kutangazwa zabuni (tender) na kushindanisha waombaji ili kupata mwekezaji bora kwa Tanzania hivyo kuvunja Katiba ya nchi na kwamba DP World imekuwa ikipambwa kwa maneno ya baadhi ya watu wakati haikushindanishwa na wengine huku akisema pia mkataba huo hauna ukomo bali ni hadi shughuli zao zitakapokoma hivyo kuiomba Mahakama kubatilisha mkataba huo ambao pia uliridhiwa na Bunge ukiwa na mapungufu lukuki.
Katika kujibu hoja hizo wajibu maombi ambao ni mawakili wa Serikali kupitia Wakili wake mkuu Mark Mulwambo inasema hoja ya kuvunjwa kwa Katiba sio ya kweli na kama ni kweli inahitaji kuthibitishwa ipasavyo hivyo dhamira ya Serikali ni njema kuwa na makubaliano yanayoitwa mkataba ambao ni rafiki kwa Taifa tofauti na taharuki inayoenezwa kwa jamii hivyo kazi kubwa ya mahakama ni kufanya uamuzi wa kubainisha ikiwa kitendo kilichofanywa na Serikali kinavunja katiba ya Tanzania.
Hivyo Mahakama itapaswa kuamua ikiwa mkataba unavunja sheria za nchi huku Wakili Kalokola wa Serikali akisema Dubai ana mamlaka kisheria kuwekeza nchini Tanzania kama mkataba wa kimataifa uliopitia michakato yote hadi kuridhiwa na Bunge.
Mwenyekiti wa jopo la majaji watatu jaji Dustan Ndunguru ameahirisha kesi hiyo hadi kesho (Julai 27, 2023) kuanzia saa tatu asubuhi ambapo Serikali itaendelea kujibu hoja za waleta maombi juu ya mkataba huo.