Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro imekusudia kuweka wazabuni katika vyanzo vyote vya mapato ili waweze kukusanya mapato mengi zaidi.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kumaliza mwaka wa fedha kwa mwezi Aprili hadi Juni 2022-2023, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Edmund Rutaraka amesema kuwa baraza hilo limeazimia kuongeza nguvu kwa kuwa na wazabuni watakao pewa lengo la makusanyo ili kufikia lengo la ukusanyaji mapato unaotamaniwa na Halmashauri hiyo .
“Kati chanzo chetu eneo la Maji moto (Chemka) kwa mwaka mmoja tunakusanya shilingi Milioni 230 na sasa mzabuni mpya tumemtaka akusanye shilingi Milioni 366 hii yote ni kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato katika vyanzo vyetu” Edmund Rutaraka Mwenyekiti Halmashauri ya Hai.
Aidha amesisitiza wakusanyaji wa mapato katika vyanzo vyote kuhakikisha wanatumia ipasavyo mashine zilizo unganishwa na mfumo wa serikali ili kuweka rekodi na kuonesha uhalisia wa kazi wanazo fanya akiongeza kuwa kwa watakao shindwa kufikia lengo wataondolewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri wa hiyo amesisitiza suala la usafi katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Bomang’ombe kwa kuwataka wananchi kutoa tozo ya taka.
“Katika kuhakikisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bomang’ombe unakuwa safi ni lazima wananchi watoe tozo ya taka kisheria,tutatoa elimu hiyo kwa wananchi wote na baada ya hapo atakaye kaidi tutamchukulia hatua kali za kisheria” Dionis Myinga Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Hai