Mamia ya wakazi wa Kijiji cha Remung’orori Wilayani Serengeti mkoani Mara wameandamana na kuwaondoa ofisini kwa nguvu Mwenyekiti, Afisa Mtendaji na Wajumbe wa Serikali ya kijiji hicho kushinikiza serikali imalize mgogoro wa mipaka kati ya Kijiji cha Remung’orori Wilayani Serengeti na kijiji jirani cha Mekomariro.
Pia wakazi hao wamezuia kufanyika kwa shughuli za maendeleo sambamba na kuifunga shule ya msingi Remung’orori pamoja na ofisi ya kijiji hicho kwa muda usiojulikana wakishinikiza serikali kumaliza mgogoro wa mipaka baina ya kijiji chao na kijiji jirani cha Mekomariro kilichopo wilayani bunda.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Ezron Msamba amesema, sababu ya yeye kutolewa katika ofisi ni kutokana na mgogoro wa ardhi uliopo kati ya Kijiji chake na kijiji jirani cha Mekomariro ambao umedumu kwa muda mrefu sana na wananchi wamekuwa wakimtuma kwa viongozi ili uweze kupatiwa utatuzi bila mafanikio.
Afisa Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Remung’orori David Makonda amesema,wananchi wamekosa uvumilivu ukizingatia suala la utatuzi wa mgogoro baina ya Kijiji hicho na kijiji jirani cha Mekomariro limekuwa likifanyiwa kazi na viongozi wa juu wa Serikali.