Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt.Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za mitaa kuzingatia utawala bora na kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Makamu wa Rais pia amewataka viongozi hao kusimamia nidhamu, maadili na uwajibikaji pamoja na kushirikiana na jamii katika kutoa elimu ya kulinda maadili ya vijana wa Tanzania.
Dkt. Mpango ametoa kauli hizo wakati alipomuwakilisha Rais Samia mjjni Arusha, kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa 37 wa jumuiya ya tawala za mikoa Tanzania – ALAT.
Dkt. Mpango amesema ni lazima watendaji na viongozi wote wa kisiasa kufanya mazungumzo ya kujenga kwa manufaa ya wananchi panapotokea hoja au mitazamo tofauti katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha amewasihi viongozi wa serikali za mitaa kutambua lengo kuu katika nyadhifa zao kuwa ni kuwaletea maendeleo wananchi na sio migogoro baina yao wenyewe.
Dkt Mpango pia amewataka viongozi wa serikali za mitaa kuheshimiana, kuwajibika na kushirikiana kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha miradi hiyo.
Kadhalika Dkt.Mpango amewahimiza viongozi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia mipaka na majukumu yao katika utendaji wa kazi ili kuepusha migogoro na miingiliano katika kuwahudumia wananchi.