Home KITAIFA MAHAKAMA YATUPILIA MBALI MAPINGAMIZI YA BANDARI, WALETA MAOMBI KUKATA RUFAA

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI MAPINGAMIZI YA BANDARI, WALETA MAOMBI KUKATA RUFAA

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imetupilia mbali maombi ya walalamikaji ambao walikuwa wakipinga Mkataba wa bandari wakidai kuwa na matatizo mbalimbali nankusema hoja zao hazina mashiko kisheria.

Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kupitia majaji watatu chini ya mwenyekiti wa jopo la majaji Dustan Ndunguru imesema hoja za waleta maombi kwenye kesi hiyo ya kikatiba namba 05/2023 ya kupinga Mkataba wa Bandari hazikuwa na mashiko kisheria kiasi cha kusitishwa kwa taratibu za mkataba huo hivyo kuamuru kuendelea kwa mchakato wa Mkataba wa kimataifa ulioingiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni ya DP World.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya na mwenyekiti wa jopo la majaji watatu Dustan Ndunguru, akisoma hukumu hiyo kuanzia saa tatu 3:43 asubuhi hadi saa 4:25 asubuhi ametupilia mbali kesi hiyo ya kupinga mkataba wa bandari kwa maelezo kwamba pamoja na mengineyo Bunge halitakiwi kuingiliwa katika majukumu yake hivyo mahakama inajizuia kufanya uamuzi kiasi cha kubatilisha mkataba huo.

Jaji Ndunguru amesema Mahakama inakubaliana na hoja ya waleta maombi, kwamba ibara za mkataba huo wa kimataifa IGA zimevunja sheria za ulinzi wa Rasilimali, kwa kupeleka migogoro nje ya nchi hoja ambayo haina nguvu na mashiko ya kutangaza kwamba mkataba huo (IGA) ni batili ikizingatiwa Serikali katika majibu yake ilisisitiza kuwa bado Serikali ya Tanzania itakuwa msimamizi kupitia TPA.

Jaji huyo amesema uandishi bora wa vifungu vya mkataba wa IGA unaweza kurekebisha vifungu hivyo kwa maeneo ambayo yanaonekana kuwa na dosari ili kuondoa dosari husika ambapo IGA itaongozwa na sheria za Tanzania na mikataba ya miradi itaongozwa na sheria za ndani (Tanzania) bali kunapotokea migogoro basi itatatuliwa nje ya nchi.

Majaji hao kwenye maamuzi yao wanakubaliana na baadhi ya hoja za waleta maombi (wananchi) lakini hakuna uzito wa kisheria kwamba mkataba huo haufai ikiwa ni pamoja na kifungu namba 64 cha sheria ya manunuzi kuwa hakikuzingatiwa ambapo mahakama inasema hakuna manunuzi yoyote yaliyofanyika lakini pia waleta maombi walipaswa kuiunganisha TPA kwenye kesi hiyo ili kujibu baadhi ya hoja na kuhusu hadhi ya nchi mahakama inasema haioni ikiwa hadhi ya nchi inashushwa wala kuhatarishwa kwa usalama wa nchi.

Katika mambo mengi yaliyoainishwa Jaji Ndunguru anasema maombi ya walalamikaji hayana mashiko na mahakama inakataa na hakutakuwa na gharama zozote kwakuwa ni shauri la kikatiba.

Baada ya Mahakama kutoa maamuzi hayo, Wakili wa kujitegemea na mmoja wa Mawakili wa waleta maombi kwenye kesi hiyo ya kikatiba Boniface Mwabukusi amesema wanakwenda kukata Rufaa kwakuwa hawajaridhika na maamuzi ya Mahakama kuu kutupilia mbali maombi yao.

Waleta maombi kwenye shauri kwa niaba ya wananchi walikuwa ni Wakili Alfonce Lusako, wakili Emanueli Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalusi waliokuwa wakiwakilishwa mahakamani na mawakili Mpoki Mpale, Wakili Boniface Mwabukusi, Phillip Mwakilima na Livino Ngalimitumba ambapo wajibu maombi walikuwa ni Waziri wa Ujenzi na uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, Katibu mkuu wa wizara ya Ujenzi,Katibu wa Bunge la Tanzania na mwansheria mkuu wa Serikali ambao wote hao walikuwa wakiwakilishwa Mahakamani na mawakili wao ikiongozwa na Wakili wa Serikali mkuu Mark Mulwambo, Wakili wa Serikali mkuu Edson Mweyunge, Wakili Hang Chang’a, Wakili wa Serikali mwandamizi Alice Mtulo na Wakili wa Serikali Edwin Wabiro ambapo sasa Serikali imeshinda hivyo itaendelea na mchakato wa mkataba wa bandari.

Previous articleDC ILEJE AWATAKA WAMAMA KUTENGA MUDA KUWANYONYESHA WATOTO
Next articleHAKUNA MRADI UTAKAO SIMAMA CHINI YA UONGOZI WA RAIS SAMIA-BITEKO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here