Home KITAIFA MADINI UJENZI NA VIWANDA YAPAISHA SEKTA YA MADINI KILIMANJARO

MADINI UJENZI NA VIWANDA YAPAISHA SEKTA YA MADINI KILIMANJARO

 

 

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mjiolojia Fatuma Kyando amesema kuwa madini ya viwanda na madini ya ujenzi yanayochimbwa katika mkoa wa Kilimanjaro yameendelea kupaisha Sekta ya Madini kutokana na ongezeko la wachimbaji wengi wa madini hayo.

 

Mjiolojia Kyando ameyasema hayo leo kwenye ziara katika eneo la uchimbaji wa madini ya ujenzi la Holili lililopo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii katika Kanda ya Kaskazini.

Akielezea mchango wa wachimbaji wa madini ya ujenzi na viwanda, Mjiolojia Kyando amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2021/2022, Ofisi yake ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 2.240 sawa na asilimia 112 ya lengo la shilingi bilioni mbili huku wachimbaji wa madini ya ujenzi na viwanda wakichangia kwa asilimia 82.6 kwa kulipa shilingi bilioni 1.849 zilizotokana na mirabaha na ada za ukaguzi.

Akielezea hali ya uwekezaji katika mkoa huo, amesema kuwa kwa sasa kuna migodi ya kati miwili na migodi midogo 200 ya wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli zao hasa katika wilaya za Rombo, Same na Mwanga na kusisitia kuwa ofisi yake inaendelea na juhudi kubwa za kuvutia wawekezaji kwenye Sekta ya Madini.

 

Akielezea mafanikio yaliyopatikana kutokana na uwekezaji huo, amesema kuwa sambamba na ongezeko la makusanyo ya maduhuli, migodi imekuwa ikichangia katika uboreshaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule, uboreshaji wa vituo vya afya pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania.

“Mfano mzuri ni mgodi wa Rock Block unaojihusisha na utengenezaji wa tofali zinazotokana na miamba ambapo awali walikuwa wakitumia teknolojia ya kawaida, kwa sasa wanatumia teknolojia ya kisasa na kuzalisha bidhaa bora ambazo huuzwa nchini Tanzania na nchi ya jirani ya Kenya, mgodi huu unaomilikiwa na mtanzania kwa asilimia 100 umetoa ajira kwa vijana wa vijiji vya jirani na mikoa ya jirani,” amesisitiza Mjiolojia Kyando.

Previous articleSPIKA TULIA ATAMBA KUTOMHOFIA SUGU _ MAGAZETINI LEO IJUMAA MEI 05/2023
Next articleSERIKALI YAJIPANGA KUMLINDA MTOTO WA KIUME DHIDI YA UKATILI WA ULAWITI.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here