Wananchi mkoani Katavi wametakiwa kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa wa malaria licha ya takwimu za maambukizi ya ugonjwa huo kupungua kwa kiasi kikubwa mkoani humo.
Akihutubia katika maadhimisho ya siku ya malaria duniani leo April 25, 2023 Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Katavi Cresensia Joseph, aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Katavi katika maadhimisho hayo amesema maambukizi ya malaria katika mkoa huo yamepungua kutoka 35% mwaka 2017 hadi 21% mwaka 2021 na hiyo yote imechangiwa na hatua madhubuti zinazochukuliwa na serikali katika kupambana na ugonjwa huo.
“Vifo vitokanavyo na malaria imepungua kutoka vifo 193 mwaka 2017 hadi kufikia vifo 34 mwaka 2022. Hii inatokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na jamii, ikiwemo matumizi sahihi ya vyandarua ambavyo hugawiwa kwa wananchi kupitia makundi mbalimbali” amesema Cresensia Joseph.
Amesema licha ya takwimu hizo kuonesha hatua kubwa iliyopigwa katika kutokomeza ugonjwa huo, wananchi wanapaswa kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kujikinga na malaria ikiwemo kudhibiti mazalia ya mbu na kutumia vyandarua vyenye dawa.
Aidha Cresensia amesema halmashauri ya wilaya ya Nsimbo inaongoza kwa kuathiriwa na maambukizi ya malaria kwa asilimia 31.6 ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Tanganyika yenye 25.6%, halmashauri ya wilaya ya Mlele 20%, halmashauri ya wilaya Mpimbwe 16% na Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda yenye 10.1%