Na MWANDISHI Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana amewasili mkoani Dodoma kuanza ziara katika mikoa ya Manyara, Mara, Simiyu na Tabora.
Akiwa katika mikoa hiyo atakagua uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuzungumza na wananchi.
Pia, atashiriki vikao vya ndani vya Chama kwa kuzungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali sambamba na mikutano ya hadhara yenye lengo la kuelezea masuala mbalimbali yanayohusu uutekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025.
Katika ratiba ya ziara ya Kinana Julai 23 ,2023 amewasili mkoani Dodoma kisha atakwenda wilayani Kondoa ambako atashiriki mkutano mkuu wa jimbo la Kondoa.
Aidha, Julai 24, 2023 Makamu Mwenyekiti Kinana atawasili wilayani Babati mkoani Manyara ambako atashiriki mkutano wa Kamati ya Siasa ya Mkoa na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Simanjiro.
Julai 25, 2023 atakwenda mkoani Mara na Julai 26, 2023 atashiriki vikao vya Chama, kukagua ukumbi wa CCM na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ukumbi huo na kisha atafanya mkutano mkubwa wa hadhara.
Aidha, Julai 27, 2023 Kinana atapokelewa Bariadi mkoani simiyu tayari kwa kushiriki mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, pia atakuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya CCM Mkoa.
Baada ya hapo atapata nafasi ya kuzungumza na waganga wa tiba asili na kushiriki mkutano wa hadhara.
Kinana atahitimisha ziara yake mkoani Tabora ambapo atapokelewa Julai 29 na Julai 30, mwaka huu atashiriki mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa na baadae mkutano wa hadhara.
Ziara hiyo ya Kinana itahitimishwa Agosti 1, mwaka huu.