Home KITAIFA KESI YA ALIYEKAMATWA NA JINO LA TEMBO YAENDELEA

KESI YA ALIYEKAMATWA NA JINO LA TEMBO YAENDELEA

 

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoani Mbeya chini ya Hakimu Zawadi Laizer imeendelea kusikiliza kesi inayomkabili January Samson Tuntuma (31) mkazi wa kijiji cha Isangawana wilayani Chunya akituhumiwa kupatikana na nyara ya Serikali (jino la Tembo) lenye thamani ya zaidi ya Sh.Million 30.

Shahidi wa upande wa Serikali aliyefika kuendelea kutoa maelezo ya jamuhuri ni Askari polisi H.695 D/C Emmanuel wa kituo cha Polisi Chunya mjini ambaye amesema Desemba 04, 2020 saa tano usiku alipigiwa simu ya mkuu wa upelelezi Wilaya ya Chunya akihitajika kazini usiku huo.

Amesema baada ya kufika alimkuta kiongozi huyo akiwa na maafisa wa wanyamapori wakiwa na mtu (January Samson Tuntuma) aliyeelezwa kuwa amekamatwa na nyara ya Serikali bila kibali hivyo aliagizwa kuchukua maelezo yake ambapo alikiri kosa kwa kueleza hadi eneo la Luwalaje Chunya ambako alipata jino la Tembo lililothaminishwa na kubainika kuwa na uzito wa Kg 3 na thamani ya Sh.Mil.34, 636, 500.

Baada ya hapo mwendesha mashtaka wa Serikali George Ngwembe na mwenzake Emelda Aluko wakaiomba mahakama kuahirisha shauri hilo hadi hapo baadaye.

Hakimu mkazi Mfawidhi katika mahakama ya hakimu mkazi Mbeya Zawadi David Laizer ameahirisha kesi hiyo hadi baadaye itakapokuja mbele ya mahakama hiyo na mshtakiwa anaendelea kuwa nje kwa dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa January Samson Tuntuma (31) mkazi wa Isangawana Wilayani Chunya anashtakiwa kwa kosa moja la kupatikana na nyara ya serikali ambayo ni jino la Tembo kinyume na kifungu namba 86 (1), (2) (c) (iii) cha sheria ya uhifadhi wanyamapori.

Previous articleWAZIRI UMMY APONGEZA UMEME WA UHAKIKA VITUO VYA AFYA
Next articleBANDARI ZA ZIWA VICTORIA ZAVUKA LENGO LA KUHUDUMIA SHEHENA, ZAFIKISHA 101% YA LENGO KABLA YA MWAKA WA FEDHA KUISHA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here