Kamati maalum ya kutatua changamoto za kibiashara nchini iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa imeanza kukusanya maoni ya wafanyabishara wa jijini Dar Es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt.John Jingu amesema kamati hiyo imepewa siku 14 kukamilisha kazi ya kukusanya maoni ya wafanyabishara kote nchini na kuwasilisha Taarifa hiyo Serikalini kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.
Dkt. Jingu amepongeza mahudhurio ya wafanyabiashara hao na namna wanavyotoa maoni yao kwa uwazi na uhuru ili kuwezesha pande zote mbili kufikia muafaka wa kutatua changamoto zilizojitokeza awali.
Kwa upande wake katibu wa kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara Dr. Hashil Abdalah amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu hivyo ipo tayari kuwapatia Wafanyabiashara hao nafasi ya kujadili kwa pamoja kero zao ili kuona nini kifanyike na kupata ufumbuzi yakinifu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Bw. Hamis Livembe amesema Kikao hicho ni kwa ajili ya kupata Mapendekezo ya nini kifanyike ivyo amewashauri Wafanyabiashara kutoa maoni na kero zao zote zinazowakabili ili Serikali iangalie namna bora ya kuweza kuwasaidia.
Kamati hiyo inayoundwa na wajumbe 14 kutoka kwa wawakilishi wa wafanyabiashara, Wizara na Taasisi mbalimbali zinazohusika na biashara nchini, imepanga kufanya mikutano kwa siku mbili kuanzia tarehe 22 na 23 Mei, 2023 Jijini Dar Es Salaam, kisha itahamia katika kanda mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar na kuhitimisha kwa kufanya majumuisho kabla ya kuwasilisha ripoti hiyo kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu.