Waziri wa Habari, mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ametangaza kuongeza muda wa Miezi sita kwa Kamati ya kutathimini hali ga Uchumi kwa vyombo vya habari na wanahabari.
Kamati hiyo awali ilipewa muda wa miezi mitatu kukamilisha ripoti yake kabla ya baadae kuomba muda zaidi, baada ya kuwashirikisha wataalamu kutoka vyuo Vikuu na Mamlaka ya TCRA.
Kamati hiyo ya watu tisa inayoongozwa na Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando ina kazi ya kupata taarifa ya hali ya waandishi wa Habari katika vyombo vya Habari wakiwemo walioajiriwa, wenye mikataba, wawakilishi mikoani na wanaoshirikiana na vyombo hivyo.
Nape amesema kazi ya kamati hiyo ni kubwa hivyo inahitaji umakini katika utekelezaji wake kwani ndiyo imebeba hatma ya vyombo vya habari na wana habari.
“Rais Samia anasubiri sana ripoti yenu hivyo mkae mkijua kuwa Taifa zima lipo kimya kusubiri mtakuja na kipi”, aliongeza Waziri Nape.
Wajumbe wa Kamati hiyo ni Katibu Gerson Msigwa,Msemaji wa Serikali, Rose Reuben Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), Joyce Mhavile Mkurugenzi Mtendaji wa ITV, Sebastin Maganga, Mkuu wa Maudhui Clouds Media Group, Bakari Machumu, Mkurugenzi Mtendaji Mwananchi Communication.
Wengine ni Keneth Simbaya Mkurugenzi Umoja wa Club za Waandishi wa Habari (UTPC) Jacquline Owiso kutoka DSTV na Mpiga picha mkongwe Richard Mwaikenda.